LIVE STREAM ADS

Header Ads

TUONEENI HURUMA. WASEMA WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI BUJORA ILIYOKO KISEMA MKOANI MWANZA.

Baadhi ya Wanafunzi wa darasa la Tano katika Shule ya Msingi Bujora iliyoko Kata ya Kisesa Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza
wakiwa wameketi chini wakiwa darasani. Hili ni moja ya madarasa yenye upungufu wa madawati hali ambayo imepelekea wanafunzi kukaa chini wakati wa Masomo. 

Pamoja na kwamba wanafunzi wa darasa la saba wamemaliza mitihani yao na wako nyumbani, bado madawati waliyoyaacha hayajaweza kusaidia katika kuziba uhaba wa madawati unaoikabiri shule hii ambayo iko Kilomita chache kutoka Jijini Mwanza.
Na George Binagi-GB Pazzo
Shule ya Msingi Bujora iliyopo Kisesa Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, inakabiriwa na uhaba mkubwa wa madawati, hali ambayo imesababisha asilimia kubwa ya wanafunzi wa shule hiyo kusoma huku wakiwa wamekaa chini.

Shule hiyo yenye wanafunzi wapatao 1,382 ina jumla ya Madawati 159 ambapo kwa wastani wa wanafunzi watatu, idadi hiyo ya madawati inatumiwa na wanafunzi wapatao 477 hali inayowaacha wanafunzi wengi zaidi wakiwa hawana madawati ya kukalia wawapo darasani ambapo upungufu uliopo kwa sasa ni wa takribani madawati 478.

Akizungumzia changamoto ya ukosefu wa madawati katika shule hiyo ya Bujora, Isack Elias ambaye ni Mwalimu Mkuu shuleni hapo amebainisha kwamba, awali waliazimia kumaliza tatizo hilo kwa wazazi kuchangia kiasi kidogo kwa ajili ya utengenezaji wa madawati lakini juhudi hizo zilikwama baada ya zoezi hilo la wazazi kuchangia utengenezaji wa madawati kusimamishwa kutokana na malalamiko ya wananchi kuwa wanaelemewa na michango ya maendeleo ya shule.

Pamoja na Changamoto hiyo, Elias amewasihi wazazi kuona umuhimu wa jambo hilo na hivyo kuridhia uchangiaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya shule kwa ajili ya manufaa ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ya Bujora.


Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Ufuatiliaji wa Miradi ya Kijiji ngazi ya Kata ya Kisesa, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dismas Kwilligwa, ameeleza kuwa suala la kumaliza changamoto zilizopo katika shule mbalimbali hapa nchini ikiwemo Bujora, haziwezi kutatuliwa na Serikali pekee hivyo ni vyema wazazi wakaona umhimu wa kuchangia huduma mbalimbali pindi zinapohitajika.

Kamati hiyo ilifanya ziara katika shule hiyo ili kujionea hali ya upungufu wa madawati uliopo katika shule hiyo, ambapo mwenyekiti wa Kamati hiyo ameahidi kuifikisha changamoto hiyo kwa wazazi kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi ili wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo waweze kujisomea katika mazingira bora.


"Mapema mwaka huu kabla ya michango mbalimbali kusitishwa katika shule hiyo kutokana na malalamiko ya wazazi, shule hiyo kwa kushirikiana na wazazi walichanga fedha ambazo ziliweza kusaidia katika kufikisha huduma ya umeme shuleni hapo ambapo lengo lililopo ni kuwa na darasa la Kompyuta kwa ajili ya kufundishia somo la TEHAMA". Alisema Kwilligwa.

Aidha tofauti na Shule nyingine ambazo zimekuwa zikionekana kukabiliwa na uhaba wa vyoo, kwa upande wa Shule hiyo ya Bujora hali inaridhisha kutokana na namna ambavyo shule hiyo kwa kushirikiana na wazazi ilivyokuwa ikijitahidi kutatua mahitaji yake kupitia michango mbalimbali, kabla ya michango hiyo kuzuiliwa ambapo kutokana na kukosekana kwa michango hiyo hali imeanza kusababisha baadhi ya shughuli kukwama.

No comments:

Powered by Blogger.