LIVE STREAM ADS

Header Ads

BAADA YA KUTIMKIA CHADEMA,VERONIKA TUHOYE AZIDI KUISAMBARATISHA NGOME YA CCM.

Veronika Method Tuhoye (Chadema).
Aliekuwa Kiongozi, Kada nguri na Mwanachama mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mwanza Veronika Method Tuhoye, ameendelea na harakati zake ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, harakati ambazo zimeonekana kutishia uhai wa CCM Mkoani Mwanza.

Akihutubia katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Jumamosi katika Tawi la Kang'anga Kata ya Mkuyuni Jijini Mwanza ikiwa ni wiki moja tu baada ya Kurejesha Kadi ya CCM na Kupokea Kadi ya Chadema, Tuhoye alibainisha kuwa kila awamu wananchi wamekuwa wakiipigia Kura CCM lakini baaya ya Uchaguzi CCM imekuwa haiwakumbuki katika masuala ya Maendeleo na hivyo kuwashauri kuacha mazoea ya kuipigia CCM Kura katika chaguzi mbalimbali zijazo.

Huku akishangiliwa na Wananchi wa Mtaa huo wa Kang'anga, Tuhoye alibainisha kuwa kwa sasa chama kinachoweza kuwatetea wananchi ni Chadema pamoja na Vyama vinginge vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na si CCM tena ambapo aliwasihi wananchi hao kuwa makini na kuachana na mazoea ya kukichagua Chama cha Mapinduzi kwa kuwa wakati huu ni wa Ukombozi na si wa kuendelea kutaabika na kero mbalimbali ambazo ni pamoja na kero ya maji, huduma za Afya ikiwa ni miongoni mwa changamoto nyingi ambazo alisema kuwa ni kero kubwa zinazotokana na uongozi wa Serikali ya CCM iliyoko Madarakani.

Hadi anatimka kutoka ndani ya CCM, Miongoni Mwa nafasi alizokuwa nazo Veronica Method Tuhoye ndani ya Chama hicho ni pamoja na Mjumbe Kamati Kuu CCM Wilaya ya Nyamagana, Mjumbe wa UWT ndani ya Mkutano Mkuu Mkoa wa Mwanza, Mjumbe baraza la Wanawake Wilaya ya Nyamagana pamoja na Mjumbe Kamati ya Siasa Kata ya Butimba Wilayani Nyamagana.

Akizungumza katika Mkutano huo, Bakary Mustafa ambae alikuwa Mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti katika Tawi hilo la Kang'anga Kata ya Mkuyuni aliwasihi wananchi wote wa Mtaa huo kushirikiana na mwenyeki aliechaguliwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita huku aliwashukuru zaidi wale waliompigia kura japo kura hizo hazikutosha na hivyo mtaa huo kunyakuliwa na mgombea kutoka ndani ya Chama cha Mapinduzi CCM.


Mbali na Viongozi mbalimbali wa Chadema waliohudhuria katika Mkutano huo wa hadhara, pia vijana wawili kati ya watatu waliofunga safari yao kutoka Mkoani Geita kwenda Ikulu Jijini Dar es salaam kwa miguu kwa ajili ya kuonana na Mh.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Jakaya Kikwete, nao pia walikuwepo kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wa mtaa huo wa Kang'anga. Vijana hao hawakuweza kuonana na Rais Kikwete baada ya kuzuiliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.


Vijana waliokuwa katika Mkutano huo ambao wiki chache zilizopita walitembea kutoka Geita hadi Jijini Dar es salaam ni Athanas Michael ambae ni Mwanaharakati na Mwenyekiti Mstaafu wa Bavicha pamoja na Khalid Seleman ambae ni Mjumbe Mkutano Mkuu Taifa wote kutoka Wilaya ya Nyamagana ambapo vijana hao walieleza kusikitishwa kwao na kitendo cha kuzuiliwa kwenda Ikulu kuonana na Rais Kikwete kwa ajili ya kumweleza changamoto mbalimbali zinazoikabili Serikali yake ikiwa ni pamoja na kumfikishia ujumbe kutoka kwa Watanzania ambao wamechoka kuonewa na wanahitaji utatuzi wa matatizo yao ambayo ni pamoja na kunyang'anywa ardhi ikiwa ni miongoni mwa mambo mengine mengi waliyokuwa wamepanga kumueleza Rais Kikwete.

Na: George Binagi-GB Pazzo

No comments:

Powered by Blogger.