LIVE STREAM ADS

Header Ads

MKURUGENZI WA JIJI LA MWANZA NA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO KATIKA MASOKO NA MINADA WAMALIZA MGOGORO WAO.

Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na Minada Mkoani Mwanza wakitoa Taarifa yao baada ya Kikao kilichofanyika jana kati yao na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Halifa Hida.
Jumuiya ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na Minada Mkoani Mwanza, imetangaza kusitisha Mgomo wake wa Kutolipa Ushuru katika Masoko na Minada yote ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza baada ya matakwa waliyoyaweka kutimizwa.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Justin Sagara alitoa kauli hiyo jana katika Ofisi za Jumuiya hiyo zilizopo Kiloleli Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza, wakati akizungumza na Wanahabari kuhusiana na kusitisha Mgomo uliokuwa umewekwa na Jumuiya anayoiongoza.

Sagara alisema kuwa Jumuiya anayoiongoza ilikuwa imeweka Mgomo wa Kutolipa Ushuru katika Masoko na Minada yote iliyo katika Wilaya ya Nyamagana (Halmashauri ya Jiji la Mwanza), kutokana na madai ya kupuuzwa na Halmashauri hiyo.

Alisema Halimashauri ya Jiji la Mwanza kupitia Mzabuni wake ilikuwa ikikusanya ushuru kwa wafanyabiashara ndogo ndogo katika Masoko na Minada lakini jambo la kusikitisha ilikuwa haitambui uwepo wao hali iliyopelekea kukosekana kwa huduma mhimu kama vile vyoo sanjari na kukithiri kwa uchafu katika Masoko na Minada wanayofanyia shughuli zao.

Baada ya hiyo, Jumuiya hiyo ilimuandikia barua Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Halifa Hida ikiomba kukutana na kwa ajili ya kumuelezea changamoto zinazowakabili na kutafuta namna ya kuweza kuzitatua ambapo jana Jumuia hiyo imekutana na Mkurugenzi huyo ambae amesema kuwa madai ya wafanyabiashara hao ni ya msingi na hivyo kuahidi kuyafanyia kazi huku akiwasili kusitisha mgomo wao wa kutolipa Ushuru.

Kufuatia hatua hiyo, Jumuiya hiyo imetangaza kuanza kulipa Ushuru katika Minada na Masoko iliyopo katika Wilaya ya Nyamagana (Halmashauri ya Jiji la Mwanza) kuanzia siku ya Jumamosi ijayo ya February 14 Mwaka huu.
Justin Sagara (Katikati) ambae ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na Minada Mkoani Mwanza wakitoa Taarifa yao baada ya Kikao kilichofanyika jana kati yao na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Halifa Hida. Kushoto ni Joseph Marcel  ambae ni Makamu Mwenyekiti na Kulia ni David Phillip ambae ni Katibu wa Jumuiya hiyo.
Kushoto ni Vivian Justin ambae ni Mjumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na Minada Mkoani Mwanza akiwa na Amos Thomas ambae ni Mtunza hazina katika Jumuiya hiyo.
Nestory Laurent (Kulia) ambae ni Makamu Mwenyekiti Kamati ya Afya katika Jumuiya ya Wafanyabiashara ndogondogo katika Masoko na Minada Mkoani Mwanza. Kushoto ni Joel Maduka ambae ni Mwandishi wa Habari Kwa Neema Radio.
Na: George Binagi-GB Pazzo.

No comments:

Powered by Blogger.