LIVE STREAM ADS

Header Ads

RATIBA YA KUUAGA MWILI WA ALIEKUWA KOCHA MSAIDIZI WA TIMU YA TAIFA SYLIVESTER MARSH YATOLEWA.

Badrudini Nsubuga (wa tatu pande zote) ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya Marehemu Kosha Marsh akitoa ratiba kamili ya Msiba wa Marehemu Marsh wakati akizungumza na Metro Fm & Binagi Media Group.
Na:George Binagi-GB Pazzo
Mwili wa aliekuwa Kocha Msaidizi wa Timu ya Taifa ya Mpira wa miguu Sylivester Marsh unatarajiwa kuagwa leo katika Uwanja wa Mirongo Jijini Mwanza, kabla ya kwenda kuzikwa katika katika makaburi ya Igoma, baada ya kuwasili Jijini Mwanza jana jioni.

Akizungumza jana na Metro Fm & Binagi Media Group, Badrudin Nsubuga ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya Marehemu Marsh, alisema kuwa shughuli ya kuuaga mwili huo inatarajiwa kufanyika leo kuanzia majira ya saa 06:00 asubuhi hadi saa 12:00 mchana katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mirongo, ambapo baadae mwili wa marehemu Marsh utapelekwa nyumbani kwao Igoma kabla ya kwenda kupumzishwa katika nyumba yake ya Milele katika Makaburi ya Igoma.

Mjane wa Marehemu Marsh Bi.Asha Sylivester Marsh alielezea kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Marehemu Mars ambapo amebainisha kuwa bado alikuwa akimhitaji zaidi Marsh kwa ajili ya malezi ya watoto ambao bado ni wadogo na wanasoma.

Zaidi aliwahusia wanamichezo nchini kufuata nyayo za Marehemu Marsh katika utendaji wake wa kazi sanjari na kuwapenda na kuwashauri vyema watu wote kubwa zaidi kupenda kuibua na kuendeleza vipaji kwa wanamichezo kama Marehemu Marsh alivyokuwa akifanya.

Nae Jumaine Shengelo ambae ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza MZFA alimuelezea Marehemu Mwalimu Marsh kuwa katika enzi za uhai wake wakati akicheza mpira, alikuwa ni kijana mtulivu na mwenye nidhamu uwanjani ambae alikuwa na mwamko wa kimichezo hali iliyomsukuma pia kuanzisha kituo cha michezo pamoja na Timu ya Soka ya Marsh Athletic Academy.

Aidha aliongeza kuwa jambo ambalo angependa kuliweka wazi ni kwamba Timu ya Marsh Athletic Academy haitakufa, kwa sababu ameacha watu ambao wataweza kuiendeleza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Nae Samiry Omary ambae ni Mchezaji wa timu ya Soka ya Marsh Athletic Academy alisema kuwa wachezaji wa timu hiyo wameupokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Marehemu Mwalimu Marsh kwa kuwa bado walikuwa wakimhitaji na walikuwa wameahidiana mambo mengi ya kimichezo ambapo wamewaomba wadau michezo wajitokeze katika kuiendeleza aliyoiacha ya Marsh Athletic Academy.

Akizungumza kwa masikitiko Makubwa Hamza Yusuph Shido ambae ni Mdau wa Michezo na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Utemini Kata ya Mirongo ulipo Msiba wa Marehemu Mwalimu Marsh, alisema kuwa wanamichezo wamesikitishwa kwa kitendo cha mwili wa Marehemu Mwalimu Marsh kusafirishwa kwa njia ya barabara (Kwa gari/ Coaster) kutoka Jijini Dar es salaam ukilinganisha nafasi aliyokuwa nayo katika Soka la Tanzania.

Alisema amesikitishwa namna Chama cha Soka Mkoani Mwanza MZFA pamoja na Shirikisho la Soka nchini TFF walivyoshindwa kumuenzi Marehemu Mwalimu Marsh hususani kwa namna mwili wake ulivyosafirishwa sanjari na katika michezo ya ligi kuu ya Tanzania bara iliyochezwa jana kushindwa kuonyesha ishara ya aina yoyote ya kumuenzi marehemu Marsh.

Marehemu Mwalimu Sylivester Marsh alizaliwa mwaka 1960 na alifariki juzi jumamosi March 14 alfajili akiwa katika Hospitali ya Taifa Mhimbili kwa ajili ya Matibabu ya Saratani ya Koo ambapo enzi za Uhai wake aliwahi kuwa mchezaji wa timu mbalimbali za soka hapa nchini ikiwa ni pamoja na Kufundisha Klabu kadhaa za Soka ambazo ni pamoja na Kagera Sugar pamoja na Azam FC ambapo pia amewahi kuwa Kocha Msaidizi wa Timu ya Taifa ya Soka.
BINAGI MEDIA GROUP: PUMZIKA KWA AMANI KOCHA MZALENDO MARSH.

No comments:

Powered by Blogger.