MANSOOR AWAHIMIZA WANANCHI WA HUNGUMALWA KUJIANDIKISHA ILI KUUNGANISHIWA NISHATI YA UMEME.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu (Kushoto) akiwakabidhi walengwa mifuko ya Simenti iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kwimba Sharif Hiran Mansoor (mwenye Kinasa sauti).
Na:George GB Pazzo
Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mkoani
Mwanza Sharif Hiran Mansoor (CCM) amewahimiza Wananchi wa Kata ya Hungumalwa
Jimboni humo, kujiandikisha kwa wingi ili kuunganishiwa nishati ya Umeme baada
ya nishati hiyo kufikishwa katika Vijiji vya Kata hiyo.
Mansoor alitoa
kauli hiyo ijumaa iliyopita wakati wa Uzinduzi wa Umeme katika Vijiji vya Kata
ya Hungumalwa, ambapo alibainisha kwamba kwa juhudi zake nishati hiyo ya Umeme
imefikishwa katika Kata ya Hungumalwa kupitia Mpango wa Umeme Vijijini.
Alisema kuwa
kasi ya wananchi kujiandikisha kwa ajili ya kufikishiwa huduma ya Umeme katika
Kata hiyo ni ndogo ambapo alibainisha kuwa Kaya 65 pekee ndizo zimeweza
kujiandikisha na kulipia gharama za kuunganishiwa Umeme, ambapo kwa kila kaya
gharama ya kuunganishiwa Umeme ni shilingi 27,000 pekee.
Kuhusu kero
ya Maji katika Jimbo la Kwimba, Mansoor alieleza kuwa kero hiyo imekwisha
tafutiwa Ufumbuzi ambapo tayari Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka
Maji Jimboni humo umekwisha kamilika hivyo kilichosalia ni Maji hayo kuanza
kusambazwa kutoka katika tenki la Maji lililopo Muhalo ili kuwafikia wananchi.
Mbali na
hayo, pia Mansoor alikabidhi Mifuko Mia Sita ya Simenti kwa ajili ya shughuli
mbalimbali za Maendeleo katika Kata ya Hungumalwa, Shilingi Milioni Tano kwa
ajili ya Kusaidia kukamilisha Ujenzi wa Zahanati ya Kata hiyo, Shilingi laki
tano kwa ajili ya Matibabu ya Mtoto mmoja alifikishwa na mzazi wake katika
kikao cha halmashauru kuu ya CCM Wilayani humo pamoja na kuvisaidia vukundi vya
ujasiriamali vya Mlimani, Ilungu, Buyogo na Tusaidiane Hungumalwa Vyelehani viwili
kwa kila kikundi kwa ajili ya Shughuli zao za Ushonaji.
Akizungumza
katika Uzinduzi huo wa Umeme katika Kata hiyo ya Hungumalwa, Katibu wa Chama
cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu alibainisha kuwa Chama hicho
kimedhamiria kufikisha maendeleo kwa wananchi huku akiongeza kuwa chama hicho kimejengeka
katika misingi ya watu tofauti na vyama vingine ambavyo amesema vimejengeka
katika misingi ya Saccos na havina dhamira ya kuwatumikia wananchi.
Nao wananchi
wa Kata ya Hungumalwa wamemshukuru Mbunge wao Mansoor kwa kutimiza ahadi yake
ya kuwafikishia nishati ya Umeme ambapo wamebainisha kuwa mbali na matumizi ya
nyumbani pia nishati hiyo itawanufaisha katika shughuli mbalimbali za
uzalishaji pamoja na kuwasaidia wanafunzi kupata mwanga bora kwa ajili ya kujisomea
na hivyo kuondokana na kero ya mwanga wa vibatari ambao ulikuwa ukiwaathiri
hapo awali.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu (mwenye miwani) akiwakabidhi walengwa mifuko ya Simenti iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kwimba Sharif Hiran Mansoor (mwenye Kinasa sauti mkononi).
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu (Kushoto) akiwakabidhi walengwa vyelehani vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kwimba Sharif Hiran Mansoor.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu (Katikati) akiwakabidhi walengwa vyelehani vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kwimba Sharif Hiran Mansoor.
Wananchi wa Hungumalwa wakiwa katika Mkutano wa hadhara uliofanyika ijumaa wiki iliyopita kabla ya uzinduzi wa Umeme katika Kata hiyo.
Msafara wa Mbunge wa Jimbo la Kwimba Sharifu Hirani Mansoor pamoja na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu ukielea katika zoezi la Kuwasha Umeme kama ishara ya Uzinduzi wa Umeme katika Vijiji vya Kata ya Hungumalwa Wilayani Kwimba.
CREDIT: RADIO METRO MWANZA
No comments: