LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWAGI SEKONDARI WILAYANI KWIMBA KUKAMILISHA UJENZI WA MAABARA HUKU IKIWA HAINA WAALIMU WA MASOMO YA SAYANSI.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu (Kushoto) akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwagi iliyopo Sumve Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza alipotembelea shule hiyo March 31 Mwaka huu ikiwa ni katika ziara yake ya siku mbili Wilayani humo. Katikati ni Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Anony Dipson.
Na:George GB Pazzo
Pamoja na juhudi za Ukamilishaji wa Ujenzi wa Maabara katika Shule ya Sekondari Mwagi iliyopo Jimbo la Sumve Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza, shule hiyo bado inakabiliwa na uhaba mkubwa wa waalimu wa Masomo ya Sayansi ikiwemo kukosa kabisa mwalimu wa somo la Physics.

Hayo yalibainishwa na Mwalimu Antony Dipson ambae ni Mkuu wa Shule hiyo mwishoni mwa mwezi uliopita, wakati wa ziara ya Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu alietembelea shule hiyo ikiwa ni katika ziara yake ya Siku mbili Wilayani Kwimba.

Mwalimu Dipson alibainisha kuwa Shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 532 pamoja na waalimu 18 inakabiliwa na uhaba wa waalimu wa masomo ya sayansi ambapo alibainisha kuwa shule hiyo ina mwalimu mmoja wa Somo la Hisabati, walimu wawili kwa kila somo kwa masomo ya Kemia na Biolojia huku ikiwa haina mwalimu hata mmoja wa somo la Physics.

Kutokana na hali hiyo, Mwalimu Dipson alieleza kuwa maendeleo ya shule hiyo katika ufaulu wa wanafunzi ni hafifu ambapo aliiomba Serikali kuona umuhimu wa kuipangia shule hiyo walimu wa masomo ya Sayansi ili kuendana na umuhimu wa uwepo wa Maabara za sayansi shuleni hapo.

Wakizungumza na Radio Metro Fm, baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha kwanza katika Shule hiyo walibainisha kuwa kutokana na uhaba wa waalimu wa masomo ya sayansi walionao shuleni hapo, wanalazimika kuchangia gharama za elimu ambazo ni zaidi ya shilingi elfu ishirini kwa mwaka kwa ajili ya kuwalipa waalimu wanaotoka nje ya shule hiyo ili kuwafundisha masomo hayo.

Kutokana na changamoto hiyo ya uhaba wa waalimu wa Masomo ya Sayansi shuleni hapo, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu, aliwashauri Waalimu kuwashawishi wanafunzi kupenda kusoma Masomo ya Sayansi jambo ambalo alisema kuwa litasaidia kupunguza tatizo la upungufu wa waalimu wa masomo ya sayansi.

Kuhusu ujenzi wa Maabara, Mtaturu alisisitiza kuwa maabara hizo zinapaswa kukamilika kwa wakati mwafaka katika kipindi cha muda ulioongezwa ili kukamilisha ujenzi wa maabara katika shule za Kata hapa nchini ambao ni hadi kufikia mwezi wa sita mwaka huu ambapo aliwaomba wazazi na wananchi wote kushiriki ipasavyo na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa ujenzi wa maabara hizo unafanikiwa.

Akiwahutubia wananchi Wilayani Kwimba katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini Ngudu, Mtaturu aliwahakikishia wananchi hao kuwa tatizo la maji Wilayani humo litatatuliwa haraka iwezekanavyo ambapo aliwasihi wananchi hao kuwa makini na baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakijali maslahi yao binafsi bila kushiriki katika kutatua matatizo yanayowakabili.


Aidha aliwataka vijana kuwa makini na kutokubali kutumika kisiasa kwa kupewa viroba na bangi na baadhi ya wanasiasa kutoka vyama vya upinzani huku akiwasihi kuendelea kukiamini chama cha Mapinduzi CCM, chama ambacho alibainisha kuwa watanzania wenye maono wamekiamini kutokana na sera zake makini na hivyo kuwataka kuondoa ndoto kwamba kitaondoka madarakani.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu (Mwenye Kofia) akikagua ujenzi wa Maabara katika shule ya Sekondari Mwagi iliyopo Sumve Wilayani Kwimba alipotembelea shule hiyo March 31 mwaka huu.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Miraji Mtaturu akiwahutubia wananchi katika Mji wa Ngudu Wilayani Kwimba Mach 30 Mwaka huu alipofanya ziara yake wilayani humo.
                                                                CHANZO:RADIO METRO

No comments:

Powered by Blogger.