LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAGUFULI ASEMA WATANZANIA WANAHITAJI MABADILIKO YA KWELI.

Na:George GB Pazzo
Chama Cha Mapinduzi CCM hii leo kimezindua Rasmi Kampeni zake za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Jangwani Jijini Dar es salaam.

Mkutano huo umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa Chama na Serikali wakiwemo viongozi wakuu wastaafu ambao ni Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba, Ali Hassan Mwinyi rais wa awamu ya pili, Benjamin Mkapa rais wa awamu ya tatu na rais wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mgombea Urais wa Chama hicho John Pombe Magufuli amesema kuwa watanzania wanahitaji mabadiliko ya kweli ya kimaendeleo na kwamba atahakikisha anawaletea mabadiliko hayo ikiwa atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Octoba 25 mwaka huu.

Amesema atahakikisha anasimamia vyema maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Ufugaji, Afya, Elimu, Ajira, Uwekezaji, Ulinzi na Usalama pamoja na Afya kama Ilani ya CCM ya mwaka 2015/20 inavyoeleza.

"Uwe CCM, CUF, CHADEMA, ADC au uwe hauna chama nitakutumikia maana naamini maendeleo ya Kweli yatatokana na Magufuli hivyo naombeni mnichague". Amesema Magufuli.

Nae Mgombea mwenza wa urais Samia Suluhu Hassan amewasihi watanzania hususani akinamama kukichagua chama cha mapinduzi na hivyo kuandika historia ya Tanzania ya kuwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Mwanamke kwa ajili ya kuwatumikia.

Amesema CCM ikiingia madarakani atahakikisha anasimamia vyema uwezeshaji kwa wanawake pamoja na kusimamia upatikanaji wa huduma za afya hususani huduma za afya ya uzazi kwa wazazi.

Umati Mkubwa wa Makada wa CCM na Wananchi wamehudhuria Mkutano huo ambapo pia wasanii mbalimbali akiwemo Diamond Platnumz, Yamoto Band, Bushoke, Peter Msechu na TOT Band wakitumbuiza huku wasanii wengine wakiwemo waigizaji wa bongo movie wakipanda jukwaani na kuimba kwa pamoja wimbo wa Taifa.

No comments:

Powered by Blogger.