LIVE STREAM ADS

Header Ads

VIONGOZI WA DINI NCHINI WATAKIWA WATAKIWA KUTOFUNGAMANA NA VYAMA VYA SIASA.

Judith Ferdinand, Mwanza
Viongozi wa dini nchini wamehimizwa kutoegemea upande wowote  wa chama cha siasa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, kwani kufanya hivyo kutawagawa waumini na hatimae kuvuruga utulivu na amani iliyopo.

Hii ni kutokana na uchaguzi wa mwaka huu kuonekana kuwa na changamoto nyingi, huku baadhi ya viongozi wa dini wakisahau majukumu yao ya kuwaongoza watu kiroho na kushabikia siasa waziwazi.

Wito huo ulitolewa juzi Wilayani Ilemela Mwanza na Mkurugenzi wa shirika la  Life Givers International (Watoa uzima), Apostle Godfrey Fungo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema viongozi wa dini, wamejaribu kwa kujua ama kutokujua, kuwagawa waumini kwa kuonyesha wazi kuegemea upande mmoja wa  chama au mgombea, suala ambalo  ni hatari kwa amani  ya nchi.

"Ni kweli  viongozi  wa dini wanaweza kuwa na mapenzi na upande fulani wa chama au mgombea, japo siyo vizuri kuonyesha wazi na kuwashawishi waumini kumpigia kura mtu au chama fulani". Alisema Fungo.

Pia alisema, katika kanisa kuna baadhi ya waumini ni wagombea kwa ngazi mbalimbali na wengine ni wanachama wa vyama tofauti vya siasa, hivyo kiongozi wa dini ukionekana una pendelea chama fulani utasababisha vurugu na amani kupotea.

Aidha alisema, viongozi Wa dini zote wanatakiwa kuwaelekeza na kuhimiza wananchi kwenda kupiga kura bila ya kufanya vurugu.

Hata hivyo aliwaomba viongozi Wa dini kuendelea kuliombea taifa amani na uchaguzi uishe salama.

No comments:

Powered by Blogger.