LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAHAKAMA YATUPILIA MBALI UTETEZI WA POLISI DHIDI YA ZUIO LA MWILI WA MAWAZO KUAGWA JIJINI MWANZA.


Mawakili wa Chadema
Na Mwandishi Wetu-Binagi Media Group
Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali utetezi wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza dhidi ya zuio lake la kuzuia  Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema pamoja na waombolezaji wengine, kufanya ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa mwenyekiti wa chadema Mkoa wa Geita Alphonce Mawazo.

Uamuzi wa Mahakama hiyo umetolea hii leo majira ya saa tano asubuhi chini ya Jaji Lameki Mlacha baada ya pande zote zinazohusika katika kesi hiyo kusikilizwa na hivyo Mahakama kuamua kuondoa zuio hilo ambalo lilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Charles Mkumbo kwa kile alichokieleza kuwa ni hofu ya kiusalama pamoja na uwepo wa mlipuko wa kipindupindu Mkoani Mwanza.

Zuio hilo limetokana na kesi iliyofunguliwa jana na Chadema, mlalamikaji akiwa ni Mchungaji Charles Lugiko ambae ni baba mdogo wa Marehemu Mawazo, kwa hati ya dharura namba 10 ya mwaka 2015 ya kuiomba Mahakama kutengua uamuzi wa polisi kuzuia ibada ya kuuaga mwili wa Marehemu Mawazo Kufanyika Jijini Mwanza.

Akizungumza baada ya mahakama hiyo kutoa maamuzi hayo, John Malya ambae ni mmoja wa mawakili watatu wa Chadema waliokuwa wakiitetea kesi hiyo,  amesema mahakama imeishauri Chadema kuwasilisha nyaraka za kuomba ruhusa ya kuendelea na ibada ya kuuuaga  mwili wa maremu Mawazo kama ratiba zilivyokuwa zimepangwa hapo awali.

Baada ya maamuzi ya Mahakama hiyo, Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe akawasihi wananchi na wafuasi wa Chadema waliokuwa wamekusanyika nje ya viwanja vya mahakama hiyo kuendelea kuwa watulivu wakati taratibu za kupata kibali cha Mahakama ili kuruhusu shughuli za kuuaga mwili wa marehemu Mawazo kufanyika.

Maamuzi ya Mahakama hiyo yamepokelewa vyema na wananchi pamoja na wafuasi wa Chadema ambao wameisihi Mahakama kutoa mapema kibali cha kuruhusu ibada ya kuuagwa mwili wa marehemu Mawazo kufanyika Jijini Mwanza kabla ya kwenda kuupumzisha katika Kijijini cha Chikobe Wilaya ya Busanda Mkoani Geita.

Marehemu Alphonce Mawazo aliuawa Novemba 14 mwaka huu Mkoani Geita na watu wasiojulikana ambapo mauaji yake yanahusishwa na uhasama wa kisiasa.

Updates

Tayari Mawakili wa Chadema wamewasilisha Mahakamani hapo nyaraka za malalamiko dhidi ya suala hilo ambapo maamuzi yanatarajiwa kutolewa kesho Mahakamani hapo.

Walalamikaji wameiomba mahakama kutoa kibali ili ibada ya kumuaga marehemu Mawazo iweze kufanyika Jijini Mwanza na kuomba kuzuia jeshi la polisi kuingilia shughuli za ibada hiyo.

No comments:

Powered by Blogger.