LIVE STREAM ADS

Header Ads

NAIBU WAZIRI WA HABARI AVITAKA VYOMBO VYA HABARI KUTOA ELIMU ZAIDI YA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Getruda Ntakije na Judith Ferdinand, Mwanza
NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Anastazia Wambura, ameviomba vyombo vya habari nchini kuendelea kuelimisha jamii kuhusu mila na desturi potofu inayochangia kuwepo kwa ongezeko la matendo ya ukatili wa kijinsia, yanayoweza kuleta athari kwa maendeleo ya mtoto wa kike.

Wito huo aliutoa jana kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani yaliyofanyikia katika uwanja wa Furahisha uliopo wilayani Ilemela, mkoani hapa, yaliyokuwa na kauli mbiu "Msichana shika hatamu" iliyolenga kumtengea mtoto wa kike uwezo wa kushiriki katika masuala mbalimbali ambayo ni elimu, uongozi na kufanya maamuzi ikiwa ni pamoja na kuweka wazi Sera ya taifa katika kuleta ustawi wa watoto wa kike  na maendeleo nchini.

Alisema, kutokana na vyombo vya habari kuwa na sauti katika jamii ni vizuri viendelee kutoa elimu kuhusu mila na desturi potofu zenye athari kwa maendeleo ya mtoto wa kike ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, kupewa kazi nzito nyumbani zinazoweza kuwanyima nafasi ya kujisomea au kuachishwa shule.

"Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari waendelee kutoa fursa ya vipindi vya kuelimisha jamii kuhusu mila na desturi potofu zenye athari kwa maendeleo ya mtoto wa kike katika nchi yetu", alisema Wambura.

Aidha aliwataka wadau wa maendeleo wahakikishe malengo yaliyowekwa na Serikali ya kumuendeleza mtoto wa kike yanafikiwa kwa kupiga vita vikwazo vinavyoweza kumkwamisha kutimiza malengo yake.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini linalojihusisha na utetezi wa haki za wanawake na wasichana, Yassin Ally, alisema, kutokana na ukatili wa kijinsia kuwa moja ya changamoto zinazowakwamisha watoto kufikia malengo yao na jamii kutokuutolea sauti, shirika hilo limezindua kampeni ya kitaifa inayoitwa" Tunaweza" inayolenga kuhamasisha wanamabadiliko 150,000 kwa Mkoa wa Mwanza.

Alisema, wanataka wafanye watu wajitokeze hadharani bila kujali lawama na vitisho, wawe wanambadiliko ambao hawataunyamazia ukatili na watachukua hatua dhidi ya ukatili wa aina zote wanaotendewa watoto wa kike na wanawake.

"Shida iliyopo ni watu kuunyamazia ukatili, tunataka tufanye watu wajitokeze hadharani bila kujali lawama, vitisho wawe wanamabadiliko ambao hawataunyamazia ukatili na watachukua hatua dhidi ya ukatili wa aina zote wanaotendewa watoto wa kike na wanawake" alisema.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Shirika la Wadada Center, linalojishughulisha na utoaji elimu juu ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia kwa vijana walioko shuleni na mtaani, Lucy Elias, aliiomba jamii iweze kuwasaidia watoto wa kike katika suala la elimu, kwani wakitambua fursa walizonazo wataweza kufikia malengo yao na vyanzo vya ukatili vitapungua.
Bonyeza HAPA Kutazama Picha za Maadhimisho hayo.

No comments:

Powered by Blogger.