LIVE STREAM ADS

Header Ads

WAJASIRIAMALI KANDA YA ZIWA WAPEWA NENO.

Ikiwa Una Habari, Tukio, Picha, Maoni au Tangazo, Wasiliana Na BMG Kwa Nambari za Simu 0757 432694 Au Email binagimediagroup@gmail.com

Judith Ferdinand,Mwanza
Wajasiriamali kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na mikoa jirani,wameimizwa kushirikiana na serikali na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO),ili kuboresha bidhaa zitakazo kidhi soko la kimataifa.

Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Leonard Masale,katika ufungaji wa maonyesho ya 14, ya viwanda vidogo na vya kati Kanda ya Ziwa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.

Masale amesema,wajasiriamali wakiwa karibu na serikali pamoja na SIDO, itawasaidia kuboresha bidhaa zao kwa kuwaunganisha na taasisi za fedha pamoja na kuwapatia mafunzo.

Pia amesema, kwa kupitia maonyesho hayo, inaonyesha jinsi wajasiriamali wanavyoweza kuzalisha bidhaa bora kwa kutumia rasimali zilizopo,pamoja na kupata fursa ya kujitangaza na elimu kutoka taasisi mbalimbali zilizoshiriki.

Hata hivyo ameiomba, SIDO iwasaidie wajasiriamali kuwaelimisha na kuwaelekeza namna ya kufungasha bidhaa,ili kuendana na soko la kimataifa na kukuza uchumi wa nchi.

Aidha ameiomba SIDO,kuwafundisha wajasiriamali waliopo sokoni namna ya kufungasha bidhaa,ili ikitokea tenda wapeleke bidhaa zilizofungashwa,sambamba na kufanya kongamano na walimu wanaofundisha stadi za Ufundi kwa ajili ya kuwajengea uwezo.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Masoko SIDO Makao Makuu Lillian Massawe amesema, wajasiriamali waendelee kuweka jitihada na wazingatie ubora katika bidhaa, ili kukua na kufanikiwa katika biashara zao.

Kadhalika amesema, zaidi ya wajasiriamali 150 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ,Mwanza,Geita,Simiyu,Shinyanga, Mara na Kagera pamoja na mikoa jirani Dar es salaam, Arusha ikiwemo Zanzibar na taasisi mbalimbali zimeshiriki katika maonyesho hayo.

Naye Meneja SIDO Mkoa wa Mara Farida Mungulu amesema, lengo la maonyesho ni kuwaibua wajasiriamali ambao wanakuwa wamajificha kwa kushirikiana na halmashauri.

Vilevile ameiomba halmashauri kuhamasisha vikundi  mbalimbali vya ujasiriamali,kushiriki katika maonyesho ili kuendeleza viwanda na kukuza uchumi wa taifa.

Hata hivyo mmoja wa washiriki wa maonyesho hayo Mkurugenzi wa Sengaboy Workshop kutoka mkoani Shinyanga Senga Silvester amesema, wamepata fursa ya kujitangaza na kujifunza kutoka kwa wajasiriamali wenzake.

No comments:

Powered by Blogger.