Ukosefu wa zahanati unavyo watesa wajawazito wilayani Magu
Wasiliana na BMG kupitia 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com kwa huduma za Habari na Mangazo.
Na Blandina Aristides, Mwanza
Mipango mikakati na matamko mbalimbali ya viongozi wa
serikali ni miongoni mwa mambo makuu ambayo huaminiwa na wananchi kwa kiasi kikubwa katika nchi
nyingi za Afrika.
Matamko hayo ambayo hutolewa kupitia nyaraka za serikali na
za kuaminika, yanawapa matumaini wananchi na kuamini kuwa, kupitia hayo,
changamoto zilizopo katika jamii zitapungua ama kuondolewa kabisa.
Tunaposema Matamko, ni azma ya serikali inayoelekeza
kufikisha malengo iliyojiwekea kwa wananchi, kupitia nyaraka mbalimbali kama vile sera, katiba, malengo endelevu ya
kidunia na sheria.
Kutotekelezeka kwa baadhi ya ahadi ama maazimio yanayotolewa
na viongozi wa serikali kunawafanya
watanzania walio wengi kutoiamini
serikali yao huku wakijiaminisha kuwa, imeshindwa kutekleza sera ambayo ndio
matamko yenye kusudi la kufikia lengo na madhumuni maalum yaliyo kusudiwa.
Sera ya afya ya mwaka 1990 na kufanyiwa marekebisho
mwaka 2007 kipengere cha 5.4.1 (b)
kinaeleza kuwa serikali itaendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi
kwa kujenga zahanati katika kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata
lakini hali ilivyo sivyo inavyoelekeza.
Tangu kutungwa kwa Sera hiyo, mpaka sasa Vijiji vya
Jinjimili na Kabale wilayani Magu havina zahanati hivyo kuwalazimu wananchi
kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 10 kufuata huduma za afya katika kijiji cha Kabila.
Takwimu toka Hospitali ya wilaya ya Magu zinaonesha
kuwa taklibani wakinamama 302 kwa mwaka 2015/2016
walijifungulia nyumbani na wengine
njiani jambo ambalo ni hatari kwa afya.
Takwimu hizo pia zionaonesha kuwa kati ya wanawake 1607
walioanza kliniki kwa kipindi cha Julai 2015-Septemba 2016, wanawake 302
walijifungulia nyumbani na baadhi yao njiani bila kuwa na msaada wowote kutoka
kwa wauguzi ama wahudumu wa afya.
Hali hiyo imepelekea baadhi ya akinamama kukumbwa na
magonjwa mbalimbali kamavile Kifafa cha mimba, Fistula na homa kali pale
wanapofika kituoni baada ya kukaa muda mrefu nyumbani wakiwa wamejifungua.
Pamoja na Sera ya Afya ya Mwaka 2007, kueleza kuwepo na
zahanati katika kila kijiji, lakini
mpaka sasa vijiji zaidi ya 40 katika Wilaya ya Magu, havina zahanati, hivyo
kulazimika kutembea umbali wa taklibani kilometa 8-12 kwa ajili ya kupata
huduma za afya iwe wakati wa jua ama mvua.
Bahati Katoro ni Kaimu Mtendaji wa kijiji cha Jinjimili
ambaye anaeleza kuwa asilimia 65 ya wananchi , hupata huduma katika kata jilani
ya Kabila kutokana na kutokuwepo huduma za afya maeneo ya karibu tangu
kuanzishwa kwa vijiji hivyo huku asilimia 35 wakipata huduma katika kata ya
Nyasato.
Takwimu kutoka katika ofisi ya kijiji cha Jinjimili zinaeleza kuwa kata ya
Jinjimili inawakazi 13,690 na kaya 1672 ambazo hulazimika kufuata huduma katika
kituo cha afya cha Kabila kilichopo kwenye kata ya Kabila yenye wakazi 15,416
na kaya zaidi ya 1000.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka vigezo na
taratibu za kuanzishwa na kupandisha
hadhi mamlaka za serikali za mitaa ambazo huanzishwa kwa kuzingatia Ibara ya
145 na 146 zinaelekeza kuanzishwashwa
kwa vyombo vya Serikali za Mitaa katika eneo la Mikoa, Wilaya, Mji na Kijiji.
Katiba hiyo, imeweka pia
vigezo vya kuzingatia katika kuanzisha maeneo mapya ya utawala ngazi za
chini za serikali za mitaa ambapo inaeleza kuwa Kitongoji kinatakiwa kuwa na
Kaya zisizopungua 50 huku Kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa
(Mamlaka za Wilaya) kikielekeza kwamba eneo la Kijiji litagawanywa katika
Vitongoji visivyozidi vitano.
Lakini pia imeweka vigezo vya kuanzisha kijiji ambapo
inaeleza kuwa kila kijiji kinatakiwa kuwepo kwa eneo la kutosha kwa ajili ya
matumizi ya wananchi kwa sasa na baadaye, vitongoji visivyopungua vitano, Idadi
ya kaya zisizopungua 250, Idadi ya watu wasiozidi 10,000 na upatikanaji wa
huduma za jamii kama vile maduka ya rejareja yasiyopungua matano (5), soko,
shule ya msingi, zahanati na kituo kidogo cha polisi.
Mpaka sasa idadi ya watu waliopo katika vijiji vya Jinjimili
na Kabale, ni kubwa ikilinganishwa na katiba inavyoelekeza lakini pia hata
idadi ya kaya zilizowekwa kwenye katiba, ni tofauti na hali ilivyo katika
vijiji hivyo.
Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Jinjimili, Bahati
Balisondole anaelezea kuwa wanawake katika kijiji hicho wanapo tembea umbali
huo hutumia muda mrefu, wakati huo hata eneo wanakokwenda kupata huduma
huzipata wakiwa wamechelewa kutokana na wingi wa watu waliopo.
Aidha wanatumia taklibani zaidi ya saa mbili mpaka kufika
kituoni na wakati mwingine hupoteza kuda huo kwenda kituoni na wasipate huduma
walizotakiwa kupata.
Uchunguzi umebaini, muda wanaoutumia kufuata huduma za afya,
hata nguvu kazi ya uzalishaji mali inakua ndogo, kwani muda mwingi wanautumia
kutembea huku shughuli nyingine zikiwa zimesimama.
Sesilia Peter, ni mmoja wa akina mama ambaye alieleza kuwa,
wakati mwingine hutumia wakunga wa jadi pale hali inapoonekana kuwa mbaya,
lakini pia haisaidii kwani wakati mwingine hata mkunga, anashindwa kuwasaidia
pale tatizo linapoonekana kuwa kubwa zaidi.
Sesilia ambaye alikutana na mwadishi wa makala hii, wiki
mbili baada ya kujifungua akiwa njiani kuelekea hospitali, alieleza kuwa baada
ya kupata uchungu, alitafuta usafiri wa baiskeli ili iweze kumfika kituoni,
lakini hali ilibadilika akiwa njiani na hatimaye akajifungua bila kufika eneo
husika.
Stela Samweli ni mama wa familia yenye watoto watatu
nanimiongoni mwa mama wajawazito ambao,
hajawahi kujifungua katika kituo chochote cha afya, badala yake amekua na
mazoea ya kujifungulia nyumbani siku zote kutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipia
usafiri wa kumfikisha kilipo kituo cha afya cha kutolea huduma.
“Tangu niolewe
nikaanza kupata watoto, kujifungulia hospitalini kwangu ni kama ndoto, na nina watoto watatu
mpaka sasa, lakini pia sijapatwa na tatizo lolote,” anasema Stela.
Marco Samweli, ni Muuguzi katika kituo cha afya cha Kabila
ambaye ameeleza kuwa, kutokuwepo kwa zahanati katika baadhi ya vijiji wilayani
Magu, kumesababisha ongezeko la watu katika kituo hicho wanaokuja kupata
huduma.
Kituo hicho kimekua
kikipokea wagonjwa kutoka vijiji vya Jijnjimili, Kabale, Kabila, Shishani,
Nkungulu na Ng’haya, huku baadhi ya wananchi wengine wakitoka wilaya jirani za
Kwimba na Bariadi mkoani Simiyu.
Taarifa za kituo cha afya cha Kabila zinaonyesha kuwa, kwa
siku kina uwezo wa kupokea wajawazito zaidi ya 10, watoto wanaoletwa kliniki
zaidi ya 25, wanaotibiwa na kurudi nyumbani zaidi ya 15 na pia wana uwezo wa
kupokea takribani wanawake sita walioko katika hatua ya kujifungua.
Hali hiyo inawapa wakati mgumu kwani hata wahudumu wanaokuwa
zamu, ni wawili tu jambo ambalo huwafanya kuwa na kazi nyingi kwa wakati mmoja.
Baadhi ya wanawake hukabiliwa na magonjwa mbalimbali ikiwa
ni pamoja na fistula, malelia kali, magonjwa ya moyo, mimba kuharibika na
kwamba wengine hukutwa magonjwa hayo yamewaathili kwa kiasi kikubwa.
Idadi hiyo ya watu wanaopata huduma kituoni hapo, ni kubwa
ikilinganishwa na watumishi waliopo, kwani wakati mwingine huwalazimu kutumia
muda wa ziada ili kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma stahiki na kurudi
majumbani mwao.
Kwa mujibu wa Marcko ambaye ni muuguzi kituoni hapo, kituo
kina Daktari mmoja, matabibu wawili, wauguzi wa nne na mabwana afya wawili huku
akieleza kuwa hata uwezo wa wodi ya akinamama ni mdogo kwani inavitanda saba yu
vya kujifungulia.
Anafafanua kuwa, hata vitanda hivyo vimebanana na wakati
mwingine inawabidi kuchukua magodoro kutoka wodi nyingine ya wagonjwa wa kawaida na kuyaweka chini ili kuhakikisha
wamama hao wanapata nafasi ya kupumzika
na watoto wao baada ya kujifungua.
Pamoja na suala la kutokuwepo kwa zahanati katika vijiji
hivyo, vilevile kuna idadi kubwa ya akina mama ambao hawana upeo mkubwa wa
elimu ya kutosha juu ya upatikanaji wa huduma bora ya uzazi kwa mama mjamzito
na hivyo, kujikuta wakiendeleza desturi, mila na mazoea ya kujifungulia
nyumbani badala ya kufika katika vituo vya afya ama zahanati.
Hali hiyo ni kawaida katika vijiji hivyo, wakisahau kuwa
kufanya hivyo, ni kuhatarisha afya zao kwa sababu huduma anayotakiwa kupatiwa
mama baada ya kujifungua, hawazipati kutokana na mazingira aliyojifungulia.
Charless Lutonja ambaye naye ni mkazi wa kijiji hicho
anaeleza kuwa hali ya wananchi wa kijijini sio nzuri kwani hata usafiri wa
kuweza kuwasaidia ili kupata huduma haraka ni shida.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Magu, Maduhu Nindwa alieleza kuwa
chanzo kikuu ni uelewa mdogo kwa baadhi ya akina mama juu ya nini afanye mara
tu anapogundua kuwa na ujauzito.
“Jamii bado ina
uelewa mdogo kwenye umuhimu wa maandalizi ya kuzuia matatizo kama hayo ya
kujifungulia njiani ama nyumbani, kwani
maandalizi yanatakiwa yaanze mwanzo angalau miezi sita kabla ya muda wa
kujifungua kufika na ikiwezekana toka siku anayojua amepata mimba,” alibainisha
Dr. Nindwa.
Baadhi ya wakinamam wa kijiji cha Jinjimili wilayani Magu, wakieleza adha wanayokumbana
nayo kutokana na umbali mrefu uliopo
kutoka nyumbani hadi kilipo kituo cha afya.
No comments: