LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wakazi wa Kirumba Manispaa ya Ilemela waungana na Diwani wao ujenzi wa madarasa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
BMG Habari
Kata ya Kirumba Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, imeanza ujenzi wa vyumba 12 vya madarasa pamoja na ofisi mbili za waalimu katika shule mbili za Sekondari zilizopo katika Kata hiyo.

Akizungumza juzi katika Shule ya Sekondari Kabuhoro kwenye uzinduzi wa awamu ya kwanza ya ujenzi huo, Diwani wa Kata ya Kirumba, Alex Ngussa alisema kuwa Kata hiyo inajenga madarasa sita na ofisi moja kwa kila shule ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi madarasani hasa wa kidato cha kwanza kutokana na ongezeko kubwa la ufaulu wa wanafunzi hao.

Alisema kuwa mradi huo kwa kiasi kikubwa unashirikisha nguvu za wananchi wa mitaa yote 12 ya Kata hiyo na unatazamiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni 50 hadi hatua ya maboma kabla ya halmashauri kukamilisha hatua ya kupaua.

Kata ya Kirumba ina shule mbili za sekondari za Kabuhoro na Kirumba ambapo ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa umegawanywa kwa kila Mtaa kujenga chumba kimoja hali inayowajengea wananchi dhana ya umiliki wa madarasa hayo pamoja na shule kwa ujumla.

Kazi hiyo pia inashirikisha watumishi wa Serikali ngazi ya Kata na Mitaa chini ya Afisa Mtendaji wa Kata, Goodluck Masatu, Afisa Elimu Kata, Mwl. Abraham Kapama pamoja na na Wajumbe wote wa Kamati ya Maendeleo ya Kata.

Diwani Ngussa aliwashukru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kwenye shughuli za uchimbaji msingi katika Shule ya Sekondari Kabuhoro na kuwasihi waendelee na moyo huo kwenye kazi zote za maendeleo ya Kata hiyo huku wakizidisha mshikamano ili kukamilisha malengo waliyojiwekea.

Akizungumzia changamoto ya viti na meza katika Shule za Sekondari, Ngussa alisema kuwa Kata ya Kirumba imefanya mikutano na wazazi wa wanafunzi wa shule zote na kuwataka kila mzazi kugharamia utengenezaji wa meza na kiti ili kumaliza tatizo hilo.
Wananchi wakishiriki shughuli ya uchimbaji msingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Kabuhoro Kata ya Kirumba.
Diwani Kata ya Kirumba, Alex Ngussa (CC) aliwaasa wananchi kuweka pembeni tofauti zao za kiitikadi na kuangalia kwanza maendeleo ya Kata yao.

No comments:

Powered by Blogger.