LIVE STREAM ADS

Header Ads

KIGOMA: Shirika la KIVULINI lapongezwa na Balozi wa Norway nchini Tanzania

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mama Elizabeth Jacobsen (pichani) amelipongeza Shirika la Kutetea Haki za Wasichana na Wanawake KIVULINI la Jijini Mwanza kwa kutekeleza vyema mradi wa kuhamasisha jamii kupinga hadharani vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wasichana na wanawake katika wilaya za Kibondo, Kakonko na Kasulu mkoani Kigoma.

Balozi Mama Jacobsen alitoa pongezi hizo jana Januari 24, 2019 akiwa ziarani mkoani Kigoma kujionea na kukagua miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali ya Norway kupitia Shirika la UN Women.

Katika ziara hiyo, pia Balozi Mama Jacobsen amekagua jengo la polisi kitengo cha Jinsia na Watoto ambalo tayari limekamilika kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii.

Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally amesema shirika hilo limewajengea uwezo wanaharakati wa kujitolea zaidi ya 200 katika ngazi ya jamii kwa ajili ya kusaidia kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa wasichana na wanawake ambao hapo awali ulikuwa haupewi kipaumbele ambapo takwimu zinaonesha kiwango cha ukatili mkoani Kigoma ni asilimia 61 huku lengo likiwa ni kufikia chini ya wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Mkuu wa Polisi kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto wilayani Kibondo, Frida Ayo amesema kitengo hicho awali kilikuwa kikitumia chumba kimoja katika jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kibondo hivyo ujenzi wa ofisi hiyo utarahisha utoaji huduma kwa wananchi ambapo ameomba ununuzi wa vitendea kazi ili kurahisisha shughuli hiyo.
Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mama Elizabeth Jacobsen (kushoto) pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Maifa nchini Tanzania, Alvaro Rodriguez (kulia) wakifuatilia jambo baada ya kuwasili wilayani Kibondo.
Mkurugenzi wa shirika la KIVULINI, Yassin Ally (kulia) akizungumza jambo wakati wa ziara ya Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mama Elizabeth Jacobsen wilayani Kibondo. 
Mkuu wa Polisi kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto wilayani Kibondo, Frida Jackson Ayo akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo la polisi kitengo cha dawati la jinsia na watoto lililojengwa kwa ufadhili wa shirika la UN Women.
Mkuu wa Polisi kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto wilayani Kibondo, Frida Jackson Ayo (kulia), akimkabidhi Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mama Elizabeth Jacobsen taarifa ya ujenzi wa jengo la polisi dawati la jinsia na watoto wilayani humo.
Wanaharakati wa shirika la KIVULINI wakifuatilia jambo kwa makini wakati wa ziara ya Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mama Elizabeth Jacobsen wilayani Kibondo. 
Shirika la KIVULINI linafanya kazi katika Kata 10 zilizopo katika wilaya za Kibondo, Kakonko na Kasulu mkoani Kigoma.
Mwonekano wa jengo la ofisi za polisi kitengo cha dawati la jinsia na watoto wilayani Kibondo lililojengwa kwa ufadhili wa shirika la UN Women.
 Balozi Mama Jacobsen akipanda mti kando ya jengo la polisi dawati la jinsia na watoto wilayani Kibondo kama ishara ya kutoa ari kwa jamii kupinga ukatili wa kijinsia kwa wasichana na wanawake hatua itakayosaidia kuwa na jamii salama na yenye maendeleo.
Mwakilishi Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Maifa nchini Tanzania, Alvaro Rodriguez akipanda mti kando ya jengo la polisi dawati la jinsia na watoto wilayani Kibondo.
Tazama BMG Online hapa chini
SOMA>>> Balozi wa Ireland atoa pongezi kwa shirika la KIVULINI
#PamojaDaimaBMG

No comments:

Powered by Blogger.