Serikali kuimarisha ustahimilivu wa mradi wa umeme mto Rufiji
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Naibu Waziri Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Sima (kushoto) akipata maelezo
ya kitaalamu juu ya hali ya mazingira katika eneo la mradi wa ujenzi wa bwawa
la kufua umeme la Rufiji Hydro Power Project kutoka kwa Dkt. Samuel Gwamaka ambaye ni Mkurugenzi
Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). Naibu
Waziri alifanya ziara ya kikazi kutembelea eneo hilo mwishoni mwa wiki.
Naibu Waziri Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Sima akiongozana na Wajumbe wa
Bodi ya Wakurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
(NEMC) baada ya kukagua eneo litakapo jengwa bwawa kubwa la kufua umeme katika
Mto Rufiji. Ujumbe huu umefanya ziara ya kikazi ya kutembelea eneo la mradi wa
ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Rufiji mwishoni mwa wiki.
Na Lulu Mussa, Morogoro
Serikali imesema itahakikisha kuwa vyanzo vya maji vinavyopeleka maji Mto Rufiji havivamiwi kwa shughuli za kilimo na kibinadamu ili Mradi Mkubwa wa kufua umeme katika bonde la Mto Rufiji uweze kutekelezeka.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Sima mara baada ya kukamilisha ziara yake katika Mikoa sita hapa nchini kwa lengo la kukagua maeneo yenye changamoto za kimazingira pamoja na kutafuta ufumbuzi kwenye ikolojia ya vyanzo vya maji vinavyo changia maji katika bonde la Rufiji.
Akiwa katika eneo la mradi litakapojengwa bwawa la kufua umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji Naibu Waziri Sima amesema amefanya ziara ya kukagua vyanzo vya maji vya Bonde la Rufiji ambavyo vinahusisha matawi matatu ya mito ambayo ni Mto Ruaha Mkuu, Kilombero, Luegu, na kutoa wito kwa wananchi kutoharibu vyanzo hivyo ili kuwa na maji ya kutosha kutekeleza mradi huo mkubwa.
Katika ziara yake Naibu Waziri Sima ameweza kutoa miongozo muhimu yenye kukuza, kulinda na kusimamia mazingira kwa namna endelevu husunan Ikolojia ya Vyanzo vya maji katika Mikoa aliyopita. Naibu Waziri Sima amesema Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa kufua umeme wa Maji wa Rufiji Hydro Power Project ambapo zaidi ya MW 2100 za umeme zitazalishwa, hivyo kulingana na ukubwa wa mradi huu ni wazi uhifadhi wa Mazingira katika vyanzo hivyo ni muhimu ukatiliwa mkazo.
“Uhifadhi wa Mazingira katika Bonde la Rufiji ni wafaida kwa pande zote hasa ustawi wa wananchi. Wananchi ndio walinzi na wahifadhi wa kwanza katika kutunza Mazingira, aidha Sheria ya Mazingira, 2004 kifungu cha 6 kimetamka wajibu wa kila mwananchi kutunza Mazingira kwamba; Mtu yeyote anayeishi Tanzania atakuwa mdau na atawajibika kutunza na kuendeleza Mazingira na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu shughuli au jambo lolote ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuathiri mazingira. Hivyo kupitia sheria hii si jukumu la Serikali pekee kusimamia uhifadhi wa Mazingira, wananchi nao wana wajibu wa moja kwa moja wa kutunza Mazingira”. Sima alisisitiza.
Bonde la Rufiji lina ukubwa wa KM2 177,420 ambazo ni sawa na asilimia 20 ya Tanzania na linapita katika mikoa 11 ya Tanzania na Wilaya 32 za Tanzania, Bonde hili ni Mashuhuri kwa Kilimo, ufungaji, uvuvi na uzalishaji wa umeme katika vituo vya Mtera na Kihansi.
No comments: