LIVE STREAM ADS

Header Ads

Dampo katika Manispaa ya Iringa lamshitua Naibu Waziri wa Maziringa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Sehemu ya dampo la Kihesa Kilolo, Manispaa ya Iringa kama linavyoonekana pichani, taka hazijateketezwa kwa kipindi kirefu na halina uzio wowote. Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Mussa Sima ametoa muda wa wiki mbili kuhakikisha eneo lote linasafishwa ili kuepuka mlipuko wa magonjwa na kulinda ikolojia ya vyanzo vya maji.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Mussa Sima (katikati) akiongea na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela (kulia) pamoja na Ritha Kabati ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa Iringa baada ya kutembelea dampo la Kihesa Kilolo lilipo katika Kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa.

Na Lulu Mussa, Iringa
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Mussa Sima ameagiza kuhamishwa kwa dampo la Kihesa Kilolo lililopo katika Kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa kutokana na kuwepo katika mazingira yasiyo rasmi.

Ametoa agizo hilo mkoani Iringa baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kukagua namna bora ya kuteketeza taka bila kuathiri mazingira na kumuagiza Mkuu wa Wilaya Iringa, Richard Kasesela kusimamia maelekezo hayo mapema iwezekanavyo ikiwa ni pamoja na kuteketeza taka zilizozagaa katika eneo hilo na kuweka katazo la watu kuingia katika dampo kwa lengo la kuokota chupa za plastiki kwa ajili ya kuziuza.

Akiwa katika eneo hilo la dampo la Kihesa Kilolo, Naibu Waziri Sima alishuhudia maji machafu yakitiririka kutoka katika dampo hilo na kwenda kwenye makazi ya watu jambo ambalo linahatarisha afya za wakazi wa maeneo ya jirani pamoja na tishio la mlipuko wa magonjwa.

Akitoa msimamo wa Serikali, Naibu Waziri Mussa Sima aliagiza kwa hatua za haraka kuwekwa utaratibu wa kudhibiti maji yanayotiririka kutoka katika dampo kwa kujenga mifereji ili kunusuru ikolojia ya vyanzo vya maji katika maeneo hayo.

"Ndugu zangu hali ni mbaya sana katika dampo hili, simamieni uteketezaji wa taka mapema iwezekanavyo, Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya namna hii, wananchi wanalipia gharama za ubebaji wa taka, zinaletwa dampo kisha mnaruhusu tena wananchi kuingia dampo, kwa maana nyingine tunakusanya taka katika mitaa na kuzirudisha tena katika mitaa, hii haikubakiki". Alisisitiza Sima.

Naibu Waziri Sima pia aliagiza eneo lililotengwa na Manispaa kwa matumizi ya dampo lililopo katika Kijiji cha Mkoga, Kata ya Isakalilo lenye ukubwa wa ekari Ishirini na tano kufanyiwa Tathmini ya Athari kwa mazingira kabla ya kuanza kutumiwa, sambamba na kulipa fidia wakazi wa maeneo hayo

Wakati huo huo, Naibu Waziri Sima alimwagiza Mratibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Godlove Mwamsojo kuhakikisha anafuatilia utekelezaji wa agizo hilo na endapo Halmashauri haitatekeleza kwa kipindi walichokubaliana hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao .

Nae Mkuu wa Idara ya Udhibiti wa Mazingira ya Uteketezaji wa taka gumu, Christian Ndenga aLIkiri kuwa takribani mwezi mmoja taka katika dampo hilo hazijateketezwa kutokana na sababu za kuharibika kwa mtambo kuzolea taka "kijiko– Wheel loader".

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema kuwa takriban tani 108 huzalishwa kwa siku katika Manispaa ya Iringa na kuahidi kusimamia zoezi la kuteketeza taka zilizopo na kuhamisha dampo ndani ya wiki mbili ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Naibu Waziri Sima.

Naibu Waziri Sima yuko katika ziara ya kikazi ya kukagua maeneo yenye changamoto za kimazingira hususan katika sekta ya afya na udhibiti wa taka ngumu pamoja ikolojia ya vyanzo vya maji vinavyo changia maji katika bonde la Rufiji.

No comments:

Powered by Blogger.