LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mkuu wa Mkoa Mbeya ang'aka ujenzi wa Hospitali ya Ileje

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela akiwa amebeba tofali kabla ya kulipigiza chini ili kujua ubora wake, matofali hayo yatatumika katika Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ileje ambapo serikali imetoa shilingi bilioni 1.5 na wananchi wanachangia nguvu kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela akikagua ujenzi wa mabweni katika shule ya sekondari ya Ileje ambapo serikali imetoa shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, madarasa na vyoo.

Na Songwe RS
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela ameutaka uongozi na watendaji wa Wilaya ya Ileje kusimamia ubora katika ujenzi wa Hospitali ya Ileje ili makosa yaliyojitokeza awali katika ujenzi wa hospitali hiyo, yasijirudie.

Brig. Jen. (Mst) Mwangela aliyasema hayo jana baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo ambapo serikali ilitoa shilingi bilioni 1.5 mwezi Disemba 2018 huku majengo yaliyo anza kujengwa yakionekana kuwa na hitilafu za baadhi ya nguzo kupinda na kuwa na nyufa.

"Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Madiwani na watendaji wote, jengo lilioanza kujengwa na kuwa na nyufa na kupinda pinda liwe funzo kwetu tuhakikishe makosa hayo yasirudie tena katika ujenzi unao endelea sasa, pia wataalamu wote msimamie taaluma zenu na hatutawavumilia endapo mtafanya tofauti", alisisitiza Brig. Jen. (Mst) Mwangela.

Aliongeza kuwa Wananchi wameitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli wa kujitolea kwa ajili ya kujiletea maendeleo hivyo basi watendaji wasiwaangushe.

"Serikali imeleta fedha na wananchi wametoa nguvu zao, halafu sisi wataalamu tuiharibu kazi, mimi siko tayari kuona kazi inaharibika, kila mtalaamu atimize wajibu wake, wataalamu wa hospitali wasimamie ujenzi uendane na mahitaji ya hospitali lakini wahandisi wasimamie ubora wa majengo hayo", alielekeza Brig. Jen. (Mst) Mwangela.

Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema licha ya ujenzi wa Hospitali hiyo kuchelwa kuanza kwakuwa serikali ilitoa fedha mwezi Disemba 2018, ujenzi huo ufanyike kwa haraka na kwa viwango ili uwe na ubora unaotakiwa na sio kufanya haraka bila kuzingatia ubora huku akiahidi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.

Aliwataka viongozi wa hospitali waliopewa fedha za ujenzi wa hospitali hiyo wawe waaminifu huku akiwataka madiwani kusimamia na kuhoji kwa kufuata taratibu ili waweze kufahamu kila senti ya fedha hizo imetumikaje pia viongozi hao watoe taarifa kwa madiwani kwani ndio wawakilishi wa wananchi ili kuepusha malalamiko kutokana na wananchi kutokuwa na taarifa sahihi.

Aidha Brig. Jen. (Mst) Mwangela alisema kuwa imefikia kipindi cha mavuno hivyo basi madiwani na watendaji wa halmashauri washirikiane katika kukusanya mapato kwani hali ya ukusanyaji mapato sio nzuri

Aliwashauri wananchi wachukue tahadhari ya kutouza sana mazao yao kwakuwa si mikoa yote imevuna vizuri hiyvo bei ya mazao inaweza kuwa nzuri zaidi hapo mbeleni hivyo wasifanye haraka kuuza chakula chao na kusisitza kuwa hilo sio katazo kwa wananchi ushauri wa kuchukua tahadhari.

Brig. Jen. (Mst) Mwangela aliwataka Madiwani wasikae na kero na malalamiko ya wananchi bali wawafikishie Wakuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa ili kero hivo ziweze kutafutiwa ufumbuzi na pia wawahimize wananchi kujitokeza na kueleza kero, maoni na malalamiko yao.

#PamojaDaimaBMG

No comments:

Powered by Blogger.