LIVE STREAM ADS

Header Ads

TASAF yawapiga msasa viongozi mkoani Mtwara

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF(aliyesimama) akizungumza kwenye kikao kazi cha viongozi, watendaji na wawezeshaji wa majaribio ya utambuzi wa Kaya za Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kilichofanyika mkoani Mtwara.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evold Mmanga (aliyesimama) akizungumza kwenye kikao kazi hicho.
Mtaalamu wa Mafunzo na Uwezeshaji wa TASAF, Mercy Mandawa akitoa maelezo katika kikao hicho.
Washiriki wa kikao kazi hizo.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho.
Na .Estom Sanga, Mtwara
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeanza mkakati wa kuwajengea uelewa viongozi, watendaji na wawezeshaji katika ngazi ya Halmashauri za Wilaya juu ya zoezi la utambuzi wa Kaya za walengwa wa mpango wa kunusuru Kaya maskini ili kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa ufanisi mkubwa.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao kazi kilichofanyika mkoani Mtwara, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga alisema zoezi hilo linakusudia kuboresha mapungufu yaliyojitokeza kwenye sehemu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo inayotarajiwa kukamilika hivi karibuni na kuwa majaribio hayo ambayo kwa kiwango kikubwa yatatumia njia ya mfumo wa kompyuta yatafanyika katika Halmashauri za wilaya ya Siha,Mtwara na Tandahimba.

Mwamanga alisema baada ya kukamilika kwa majaribio hayo, kazi ya kutambua Kaya za walengwa watakaojumuishwa kwenye mpango itafanyika nchini kote ili kutekeleza maagizo ya Serikali ya kujumuisha maeneo yote kwenye shughuli za Mpango. 

Katika Awamu ya kwanza ya mpango serikali kupitia TASAF imeweza kutekeleza Mpango huo kwa asilimia 70 ya Mitaa/ Vijiji/ Shehia na hivyo asilimia 30 iliyosalia itakamishwa katika sehemu ya pili ya mpango itakayotekelezwa kwa takribani miaka mitano ijayo.

Alisema mkazo mkubwa katika sehemu ya pili ya mpango imewekwa zaidi katika kuhamasisha walengwa wa Mpango kufanyakazi kwenye miradi ya maendeleo watakayoiibua na kisha kulipwa ujira ili waweze kujiongezea kipato na kupunguza adha ya umaskini.

"Tumeweka mkakati bora zaidi ya kutekeleza maagizo ya serikali ya kupunguza dhana ya walengwa wa mpango kuwa tegemezi" alisisisitiza Mwamanga.

Aliwahimiza viongozi, vatendaji na wawezeshaji kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwenye mikutano ya utambuzi wa Kaya za walengwa ili kuondoa uwezekano wa Kaya zenye uhitaji kutojumuishwa kwenye mpango na hivyo kuondoa manung’uniko baada ya kuanza kwa sehemu ya pili ya Mpango unaotarajiwa kuzifikia takribani Kaya milioni 1.3 ikilinganishwa na Kaya Milioni 1.1 zilizoandikishwa katika sehemu ya Kwanza.

Mwamanga alisema kutokana na usimamizi thabiti wa Serikali katika utekelezaji wa mpango wa kunusuru Kaya maskini, kumekuwa na mafanikio makubwa kwa Kaya za walengwa kuanza kuboresha maisha yao huku sehemu kubwa ya kaya hizo zikitumia fursa ya kuwemo kwenye mpango kuanzisha shughuli uzalishaji mali jambo ambalo amesema limeendelea kuvutia Wadau mbalimbali wa maendeleo kutaka kuchangia zaidi raslimali fedha na utaalam.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evold Mmanda alisema TASAF kwa kiwango kikubwa imekuwa kielelezo bora cha kuwafikia wananchi wanaoendelea kuishi katika mazingira ya umaskini kutokana na namna walengwa wa mpango wa kunusuru Kaya maskini walivyotumia fursa hiyo kupunguza athari za umaskini.

Mmanda aliwataka viongozi katika maeneo ya utekelezaji wa shughuli za mpango kuendelea kuwahamasisha wananchi kuuchukia umaskini kwa vitendo jambo ambalo amesema linawezekana ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake.

No comments:

Powered by Blogger.