LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wananchi walia na gharama za JUMEME

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com 
Na Judith Ferdinand, BMG
Wakazi wa Kisiwa cha Iramba kilichopo Kata ya Mazinga Wilaya Muleba mkoani Kagera, wameiomba kampuni ya kusambaza umeme wa jua (Jumeme),  kuwapunguzia gharama za kupata huduma hiyo kutoka shilingi 3,500 kwa yuniti (unit) moja hadi shilingi 500.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Iramba kisiwani humo, Novatus Benardo alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki hafla ya uzinduzi wa mradi wa "Micro Power Economy Tanzania Roll Out" unaotekelezwa na kampuni ya Jumeme kwa ushirikiano wa karibu na Umoja wa Ulaya ukilenga kuwaunganishia wananchi huduma ya umeme jua.

Bernardo alisema wakazi wa Kisiwa hicho wamepokea vizuri mradi huo na kuhamasika japo changamoto iliyopo ni gharama ambapo yuniti moja ya kampuni ya Jumeme ni mara 13 ya umeme wa shirika la umeme Tanzania (Tanesco) hatua ambayo wananchi wa kipato cha chini hawawezi kumudu gharama.

"Mwitikio ni mkubwa kwani bei ya kusambaza umeme siyo kubwa lakini kikwazo ni bei ya uniti, tangu wawashe umeme kwa majaribio ni mwezi mmoja sasa ambapo watu walikua wameanza kununua majokofu kwa ajili ya kuhifadhia samaki, vinywaji baridi pamoja na wengine kuanza kuleta vifaa vya kutengenezea mashine za kusagia nafaka ila kwa sasa wamesitisha mpaka pale watakapo pata mwafaka wa bei nafuu za yuniti" alisema Bernardo.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Mazinga, Alex Bakenyera alisema Kijiji hicho kina Kaya zipatazo 800 zinazohitaji umeme na zilizofungiwa ni Kaya 280 hivyo aliomba waendelee kusambaza huduma hiyo ili kuzifikia Kaya nyingi na kunufaika na shughuli za maendeleo.

Naye Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa, George Mhina akitolea ufafanuzi suala la bei za huduma ya nishati ya umeme jua, alisema awali mamlaka hiyo ilikua haina kanuni ya kuwadhibithi wawekezaji wanaozalisha umeme wa k/watt 100 lakini baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu gharama wameandaa kanuni hizo na kwamba ziko mbioni kuchapishwa ili kuanza utekelezaji.

Mhina alisema kwa miezi mitatu kampuni ikiwemo ya Jumeme itatakiwa kuleta mpango kazi wake ambao utaonyesha gharama za yuniti, hivyo aliwatoa hofu wananchi kwa kuwaahidi kufanyia kazi suala hilo na kwamba watapanga bei rafiki ambayo itamnufaisha mwekezaji pamoja na wananchi.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Jumeme, Profesa Costa Ricky Mahalu alisema mradi huo unafungua fursa ya wananchi wa visiwani kufanya biashara mbalimbali ikiwemo kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo mashine za kusaga na kukoboa nafaka, viwanda vya kutengeneza mikate, viti, meza na nyinginezo na hivyo kuwasihi wananchi kuilinda miundombinu yake ili mradi uendelee kutoa huduma.

No comments:

Powered by Blogger.