LIVE STREAM ADS

Header Ads

CCM yaonya makundi uchaguzi ujao

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Baltazar Mashaka
Imebainika kwamba makundi ya baadhi ya viongozi wasaka vyeo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, yalikigharimu chama hicho kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Aidha inaelezwa kwamba wana CCM katika Kisiwa cha Ukara wilayani humo waliupokea na kuubeba msiba usio wao uliosababisha baadhi ya Vitongoji, Vijiji, Kata na Jimbo la Ukerewe kuangukia mikononi mwa chama cha upinzani wasichokijua kwa undani.

Hayo yamesemwa na Katibu CCM Mkoa Mwanza, Salum Kalli wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wanachama wa chama hicho katika Kata nne za Bwisya, Nyamanga, Bukiko na Bukungu kisiwani Ukara.

Alisema kwenye chaguzi za Serikali za Mitaa mwaka mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, CCM iliangushwa na makundi ya wasaka vyeo waliokosa kura za kutosha kwenye uchaguzi wa ndani na hivyo wakaamua kununa na kugeuka makuwadi wa upinzani na kusababisha CCM ikapoteza jimbo pamoja na baadhi ya Kata, Vijiji na Vitongoji.

Kalli alisema wanachama wa CCM waliamua kuwapa kura CHADEMA wakishirikiana na wananchi wasio wana CCM na hivyo kuuza jimbo kwa kumchagua mgombea wa CHADEMA ambaye hata hivyo alipokosa pa kuzikia msiba huo aliamua kuuachia na kurejea CCM.

Alidai CCM iliadhibiwa na wanachama wake walioshindwa kwenye kura za maoni kwa msemo wa bora tukose wote na hivyo kuonya kwamba chaguzi zijazo asitokee mtu ambaye kura hazitatosha aseme bora amwage mboga, yeye abaki na ugali kwani cha moto atakiona.

"Simlaumu mbunge, kura alizopata wana CCM walimpa wenyewe kwa sababu ya makundi ya wale ambao kura hazikutosha. Walihangaika na kuwa makuwadi wa vyama vingine, mchana walikuwa CCM, jioni NCCR-Magauni (Mageuzi) usiku CHADEMA. Ndiyo yaliyotokea Bukiko, Ukara na Ukerewe" alisema Kalli.

Alisistiza kuwa misiba waliyoibeba ya kuchagua wagombea nje ya CCM ilisababisha mbunge huyo wa CHADEMA, Josephat Mkundi kuishia katikati ya safari baada ya kubaini alidanganywa na hivyo kuamua kujiunga na CCM.

"Nguvu kubwa ya wana CCM ilimsaidia kumbeba Joseph Mkundi kushinda ubunge jimbo la Ukerewe lakini kwenye tukio la ajali (Kivuko cha MV. Nyerere) hakuna kiongozi wa chama chake aliyeshiriki na kujikuta akipwaya. Pia kutokana na kasi ya maendeleo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli na nguvu kubwa ya CCM iliyombeba, aliamua kujiunga na timu ya kuleta maendeleo" alisema Kalli.

Nao baadhi ya wana CCM wilayani Ukerewe walisema makundi nayotokana na uchaguzi wa ndani bado yapo hivyo ili chama kiibuke na ushindi ni lazima makundi hayo yaliyokigharimu chama mwaka 2014 na 2015 yatafutiwe dawa na yavunjwe.

No comments:

Powered by Blogger.