Header Ads

TCCIA yaomba vikwazo vya utoaji Stempu kwa wafanyabiashara kutatuliwa

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com 
Judith Ferdinand, BMG
Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) wameomba stempu za kielotroniki za biashara zitolewe kila Mkoa hapa nchini ili kurahisisha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara na wajasiriamali.

Akizungumza katika ufunguzi wa maonyesho ya 14 ya Biashara Afrika Mashariki yanayoandaliwa na TCCIA, Mwenyekiti wa chemba hiyo Elibariki Mmari alisema mfanyabiashara akitaka stempu za kieletroniki analazimika kuifuata jijini Dar es salaam kwani hakuna ofisi katika mikoa mingine.

Mmari alisema ili kuondoa usumbufu na gharama kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wanaomba Serikali iweke ofisi za kutolea stempu hizo TRA kila Mkoa.

"Wajasiriamali wote wanaotumia stempu hizo wanapaswa kuzifuata Dar es salaam, ambapo kutoka katika jiji hilo hadi Mwanza ni mbali hivyo kwa wale wenye viwanda vidogo na vya kati ni mzigo mkubwa na kufanya gharama za uendeshaji kuongezeka,hivyo naiomba Serikali stempu hizo zitolewe katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) za mikoa" alisema Mmari.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Edwin Rutageruka ambaye alimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema Serikali ipo mstari wa mbele kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya biashara katika mazingira mazuri na wezeshi.

"Sekta ya viwanda vidogo imetoa ajira kwa watanzania zaidi ya milioni 8,hivyo Serikali itaendelea kuwezesha viwanda hivyo ili viendelee kutoa ajira na kukuza uchumi wa nchi" alisema Rutageruka.

No comments:

Powered by Blogger.