LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali yatakiwa kutambua mchango wa AZAKI kimaendeleo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com 
Judith Ferdinand, BMG
Serikali imeombwa kushirikiana na Asasi za Kiraia (AZAKI) kufanya tafiti mbalimbali zitakazosaidia kubaini mchango wa Asasi hizo nchini katika kuchangia maendeleo ya Taifa.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko aliyasema hayo Mkutano wa tano wa Jukwaa la Wakurugenzi wa AZAKI nchini uliofanyika jijini Mwanza kwa siku mbili kuanzia Oktoba 13, 2019.

Soko alisema AZAKI zimekuwa zikifanya kazi kwa muda mrefu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 kwa mujibu wa Sheria, lakini mchango wake kimaendeleo hautambuliki vyema hivyo pamoja na mambo mengine mkutano huo ulilenga kujadili namna Serikali inavyoweza kutambua umuhimu wa AZAKI kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, maji, kilimo, uchumi pamoja na watoto.

"Mashirika yanafanya kazi kubwa lakini hata siku moja huwezi kusikia kwenye usomaji wa bajeti ya Serikali kuwa Asasi za Kiraia zimechangia kwa asilimia fulani, hali hiyo inatufanya tujihisi wanyonge na wakati mwingine inatukatisha tamaa katika shughuli zetu, hivyo tunaisihi Serikali kushirikiana na sisi ili tutanye kazi kwa pamoja" alisema Soko na kuongeza;

"Na wakishatambua hivyo basi itakuwa motisha kubwa kwa Asasi hizo na sisi tutatimiza wajibu wetu kwa kuhakikisha tunaisaidia Serikali yetu kuchakata maendeleo kwa pamoja ili tuwe na jamii inayopata maendeleo kupitia sekta mbalimbali" alisisitiza Soko.

Aidha Soko alisema Asasi za Kiraia zinafanya kazi kubwa kuanzia ngazi ya chini ya Serikali za Mitaa kwa kufuatilia masuala mbalimbali kama vile Uukatili dhidi ya wanawake na watoto ambapo kazi hizo zilipaswa kufanywa na Serikali ila kwa vile wao ni wabia kwa Serikali wanafanya kazi hizo. 

Akihitimisha mkutano huo, Kamishina wa Sera za Bajeti wa Wizara ya Fedha na Mipango, Shogholo Msangi alikiri kwamba AZAKI zimekuwa na mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo nchini ingawa lakini bado sekta hiyo haijaweza kurekodi vizuri mchango wake katika maendeleo ya nchi kutokana na sekta hiyo kuongozwa na Sheria tofauti tofauti huku pia usajili na utendaji kazi wake ukiwa chini ya taasisi tofauti tofauti za Serikali.

"Ni wakati mwafaka kwa AZAKI nchini kushirikiana na Serikali katika kufanya tathimini ya kina na kuona ni kwa namna gani kutakuwa na utaratibu mzuri wa kupima mchango wa AZAKI hizo katika kuchochea maendeleo ya Taifa" alisema Msangi.

No comments:

Powered by Blogger.