LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mkuu wa Wilaya Ilala akagua ujenzi wa soko la Kiwalani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Na Azmala Said, Dar 
Wakazi wa Kata ya Kiwalani jijini Dar es salaam wameishukru na kuipongeza Serikali kwa kuanza ujenzi wa soko kubwa ambalo baada ya kukamilika litaongeza fursa ya wao kufanya biashara zao kwa ufasaha na hivyo kujiimarisha kiuchumi.

Ujenzi wa soko hilo unaogharimu zaidi ya Tsh. Milioni 600 unatekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kupitia Mradi wa Uboreshaji Miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Baadhi ya wakazi wa Kata hiyo wametoa shukrani zao katika ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa soko hilo.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi hao, Diwani wa Kata hiyo Kiwalani, Kassim Mshama kutoka Chama cha wananchi (CUF) aliishukru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ukiwemo ujenzi wa soko hilo, barabara kwa kiwango cha lami pamoja na utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya ujasiriamali.

"Tunaipongeza Serikali kwa ujenzi wa soko hili ambalo litatoa ajira kwa wafanyabiashara kutapata sehemu bora ya kufanyia biashara zao na pia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami pamoja na utoaji wa mikopo ambapo kwa Kata yetu vikundi 10 vimekopeshwa bajaji 10" alisema.

Naye Salma Nkoloma ambaye ni mkazi wa Kata hiyo alisema ujenzi wa soko hilo utakwenda kuwatatulia changamoto mbalimbali. 

"Soko hili litakapo kamilika litakuza uchumi wetu kwani asilimia kubwa hapa tunapoishi kwa kutegemea biashara hivyo tunaishukuru Serikali kwa hatua hiyo" alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alisema ujenzi wa soko hilo unatokana na kasi ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanajengewa mazingira bora na wezeshi kiuchumi.

"Soko ili hakikisheni linajengwa kwa ubora kwani leo nimekagua lakini nitarudi kuangalia mmefikia wapi kwani lengo letu mpaka kufikia mwezi Disemba mwaka huu tunataka miradi yote iwe imekamilika"alisema Mjema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Jumanne Shauri alisema mkakati uliopo ni kuhakikisha wafanyabiashara wote waliokuwa wanafanya biashara katika eneo hilo wanapata nafasi pindi soko hilo litakapokamilika.

"Soko ili tunataka litakapo kamilika watu wa kwanza kufanya biashara hapa wawe ni wafanyabiashara ambao walikuwepo tangu awali" alisema Shauri.

Hata hivyo Mhandisi anayesimamia mradi huo John Magulu alimuahidi Mkuu wa Wilaya Ilala, Sophia Mjema kuwa hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu soko hilo litakuwa limekamilika.

No comments:

Powered by Blogger.