LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mimba na ndoa za utotoni bado ni changamoto mkoani Shinyanga

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Zainab Telack akifungua kikao cha mwaka cha kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kudhibiti Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kilichohudhuriwa na wadau mbalimbali wanaotekeleza afua za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupitia nyenzo ya MTAKUWWA. 
Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Zainab Telack (katikati) akizungumza kwenye kikao hicho. Kulia ni Katibu Tawala Mkoa Shinyanga, Albert Msovela na kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa Shinyanga, ACP Richard Abwao.
Katibu Tawala Mkoa Shinyanga, Albert Msovela (katikati) akitoa salamu zake kwenye kikao hicho.
Wadau wakimsikiliza, Katibu Tawala Mkoa Shinyanga, Albert Msovela.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Shinyanga, Tedson Ngwale akizungumza akifafanua jambo kwenye kikao hicho.
Wadau wakimsikiliza Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Shinyanga, Tedson Ngwale.  Kamanda wa Polisi Mkoa Shinyanga, ACP Richard Abwao akizungumza kwenye kikao hicho. Wadau wakimsikiliza Kamanda wa Polisi Mkoa Shinyanga, ACP Richard Abwao.

Na Kadama Malunde, Malunde 1 Blog 
Imeelezwa kuwa licha ya kuwepo kwa taasisi nyingi na jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali kwa kushirikiana na serikali bado hali ya ndoa na mimba za utotoni si shwari mkoani Shinyanga. 

Hayo yalisemwa Oktoba 11, 2019 na Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Zainab Telack wakati akifungua kikao cha mwaka cha Kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kudhibiti Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kilichohudhuriwa na viongozi wa dini, wajumbe wa MTAKUWWA na wadau mbalimbali wanaotekeleza afua za MTAKUWWA.

Telack alisema hali ya mimba na ndoa za utotoni bado si shwari mkoani Shinyanga kutokana na kwamba vitendo vya kuozesha watoto wa kike vinaendelea kwa usiri mkubwa na watoto wa wanaendelea kupewa mimba katika umri mdogo kutokana na mila potofu zinazochangiwa na ukosefu wa elimu.

"Shinyanga ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango juu cha ushamiri wa mimba na ndoa za utotoni. Naomba mtumie fursa ya kikao hiki kujadili kwa kina na kudadavua sababu zinazotukwamisha kushindwa kutokomeza mimba na ndoa za utotoni na kuweka mikakati inayotekelezeka.Kikao hiki kiwe na tija na manufaa ya kumsaidia na kumkomboa mtoto wa kike" alisema Telack.

Aidha aliwataka wadau zikiwemo taasisi na mashirika, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuongeza kasi ya kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Katika hatua nyingine Telack alisema bado kuna changamoto ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ambapo wanawake na watoto ndiyo waathirika wakubwa kutokana na uwepo wa mila na desturi gandamizi dhidi ya wanawake hali ambayo kikwazo kikubwa cha kuwanyima fursa wanawake na watoto katika kufanya maamuzi kuhusu maisha yao.

Telack aliziagiza mamlaka zote zinazohusika katika kuzuia na kupinga ukatili wa kijinsia kuendelea kuelimisha jamii kwa kutoa ufafanuzi wa athari za unyanyasaji na ukatili wa kijinsia,kusimamia haki,kuharakisha utekelezaji wa mashauri ya kesi zinazohusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Hata hivyo Telack alisema kutokana na umuhimu wa kutatua changamoto za ukatili dhidi ya wanawake na watoto hususani mimba na ndoa za utotoni, Mkoa Shinyanga umeandaa Mpango Mkakati wa Kudhibiti Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto utakaozinduliwa rasmi mwishoni mwa Mwezi Oktoba 2019 ili kukomesha matukio ya aina zote za ukatili.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa Shinyanga, ACP Richard Abwao alisema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni kesi za ubakaji kuchelewa kufikishwa kwenye madawati ya jinsia na watoto na kukosa ushirikiano hususani kwenye matukio ya kubakwa ambapo kwenye hatua za mwanzo ushirikiano huwa unakuwepo lakini baadaye wahusika kugeuka na kumaliza kesi kifamilia. 

"Kesi nyingi za ukatili wa kijinsia zimekuwa zikikwama kutokana na wahanga kuficha ushahidi, kuwakataa watu waliowafanyia ukatili mfano wabakaji na watu wanaowapa mimba watoto, familia kutorosha mashahidi, kesi kumalizwa kifamilia hali inayochangia vitendo vya ukatili kuendelea katika jamii" alisema na kuongeza;

"Baadhi ya viongozi ngazi ya jamii wakiwemo wa Vitongoji, Vijiji na Kata wamekuwa wakiongoza maridhiano kwenye familia kuhusu matukio ya ubakaji. Tunawaomba wawe wanatoa ushirikiano ili tusafiri kwa pamoja katika kukomesha vitendo vya ukatili katika jamii" alisisitiza Kamanda Abwao.

No comments:

Powered by Blogger.