LIVE STREAM ADS

Header Ads

Madiwani Tarime Vijijini wahoji zilipo fedha za asilimia 10

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Na Helena Magabe, Tarime
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Tarime Vijijini mkoani Mara wameeleza kutofahamu namna fedha za asilimia mbili zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo zilivyowanufaisha watu wenye ulemavu kama ilivyo takwa la kisheria.

Madiwani hao akiwemo Marwa Marigiri kutoka Kata ya Binagi walionyesha hofu hiyo kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo na hivyo kutaka kujua namna zilivyotumika na walengwa walionufaika.

“Haiwezakani zitumike shilingi milioni 12 ndani ya miaka mitano iliyopita kwa vikundi viwili pekee vya Walemavu” alihoji Marigiri huku akitaka pia kujua namna asilimia 10 ya fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii zilivyotumika.

Diwani huyo ambaye pia ni mlemavu wa jicho moja alisema hatasita kuwawakilisha walemavu wenzake na kuhoji namna fedha wanazostahili kupata kupitia vikundi vya wajasiriamali zilivyotumika na pia walionufaika.

Naye diwani wa Kata ya Kemambo, Rashid Bogomba alisema katika kikao kijacho ni vyema majibu ya kina na uhakika yakapatikana kuhusiana na matumizi ya fedha za asilimia 10 zinazotokana na mapato ya Halmashauri hiyo kwa makundi maalum ya wanawake, vijana na walemavu kutoka Kata zote 26.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Bumera, Deogratius Ndege alisema asilimia 10 ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii takribani shilingi milioni 290 inayopaswa kutolewa kama mikopo kwa makundi maalum haijulikani inakoenda.

“Katika Kata yangu kuna walemavu zaidi ya 30 lakini bado hawajanufaika nah ii mikopo, lazima tujue hizi fedha zinaenda wapi” alihoji diwani wa Kata ya Kiore, Rhobi John.

Mwenyekiti wa Halimashauri ya Tarime Vijijini, Simion Kelesi Samweli alisema changamoto nyingine iliyopo ni vikundi vya akina mama vinavyopaswa kunufaika na mikopo kutoka Halmashauri hiyo kuingiliwa na wanaume na hivyo kutowanufaisha walengwa na kuomba elimu zaidi kutolewa ili kuondoa hali hiyo.

Akijibu hoja hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Halimashauri hiyo, Dkt. Peter Nyanja bado kuna mwitikio mdogo kwa walengwa wa mikopo ya silimia 10 hususani wenye ulemavu na hivyo kuwasihi madiwani hao kuwahamasisha kuunda vikundi ili kunuaika na fedha hizo.

“Baadhi ni wabishi, hawapendi kukopa fedha hizi kupitia vikundi kwani kila mtu anataka kukopa peke yake. Pia kuna changamoto katika kurejesha mikopo hiyo ambapo mwaka jana katika Kata ya Nyamongo tulitoa shilingi milioni 30 kwa watu wenye ulemavu lakini hadi sasa hawajarejesha” alieleza Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii, Antony Magoti.

No comments:

Powered by Blogger.