LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kondom za bure zazua balaa kwenye kikao cha Madiwani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Na Helena Magabe, Tarime
Madiwani wa Halmashauri ya Tarime Vijijini mkoani Mara wameomba takwimu za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ziwekwe wazi kwa lengo la kutambua ni maeneo gani yenye kiasi kikubwa cha maambukizi ili wananchi wachukue hatua ya kujikinga.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Makamu Mwenyekiti wa Halimashauri hiyo, Victoria Mapesa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya UKIMWI kusoma taarifa ya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani 2020 ambapo alisema kondom 37,150 zilitolewa kwa wananchi.

Aliongeza kuwa idadi hiyo ya kondom iliwafanya madiwani kuhoji ni wapi zilipo kondomu hizo na kutaka kujua ni nani aliyegawiwa.

Diwani wa Kata ya Nyarero, John Muhabasi alihoji zilipo kondom zinazopaswa kugawia bure kwa umma na kutaka ziwekwe kwenye ofisi za kata, mahospitalini na mahotelini ili watu wajikinge na VVU.

Naye diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard alihoji zilipo kondom hizo kwa madai kuwa zinaletwa kwa lengo la kusaidia wananchi lakini matokeo yake zinauzwa kwenye maduka binafsi ya madawa muhimu.

Alisema inasikitisha kondom za MSD ndizo ziko madukani na kushauri kwamba Serikali inapotoa kondomu kwa ajili ya wananchi ni bora zikagawanywa kwenye mahoteli pamoja na nyumba za kulala wageni (guest).

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Ganyange, Sinza Keheta aliomba takwimu za maambukizi ya VVU zitajwe kama zinaongezeka ama zinapungua.

Alisema Kondom zinazouzwa madukani asilimia kubwa hazina ubora nyingine zinanuka vibaya, nyingine hutoboka wakati wa kujamiana na nyingine hubakia kwa wanawake wakati wa tendo hilo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya Tarime, Dkt. Joseph Ngowi aliwashauri wananchi wasiamini kondom za kununua madukani kwani nyingi hazina ubora.

Alisema ni bora wananchi wakaendelea kutumia kondomu za MSD ambazo ni za Serikali ama ambazo zimethibitishwa na TBS.

"Tatizo watu sio wastarabu, tulikuwa tukiweka maeneo kama ya ATM lakini ustarabu ni mdogo kwani wengine walikuwa wanachukua zote na pengine ndio wanaouzia wenye maduka ya dawa" alihoji Dkt. Ngowi.

Katika Wilaya Tarime baadhi ya maeneo yanatajwa kuwa na ongezeko kubwa la VVU kutokana na shughuli mbalimbali ikiwemo uchimbaji madini pamoja na uvuvi ambapo maeneo hayo ni pamoja na Nyamongo, Sirari, Nyamuhanga pamoja na Tarime Mjini.

No comments:

Powered by Blogger.