LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wanasheria wakumbushwa wajibu wa kuwasaidia watoto

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Wazazi na walezi nchini wametakiwa kutanguliza uhai wa mtoto kwanza katika utekelezaji wa sheria mbalimbali na kuomba msaada wa tafsiri wa sheria hizo kabla ya utekeleza wake.

Afisa Sheria Mwandamizi kutoka TACAIDS, Miraji Mambo aliyasema hayo wakati akitoa ufafanuzi wa Sheria ya UKIMWI na Haki za Binadamu kwenye mafunzo kwa watu wanaoishi na VVU kutoka mikoa ya Kagera, Mwanza, Kigoma, Tabora, Mara na Shinyanga.

Mambo alisema wananchi lazima wajifunze juu ya sheria za nchi zilizopo na linapokuja suala la kutafsiri sheria ni vyema kuwa tumia wanasheria na mawakili ili kupata tafsiri halisi kuhusiana na sheria husika.

"Lazima mjue ule msemo unaosema sheria ni msumeno yaani unakata pande mbili, kwa maana hiyo unaweza kuigeuzageuza na ukapata maana tofauti zaidi ya mbili katika sheria moja" alisema Mambo.

Awali mshiriki wa mafunzo hayo ya Sheria ya UKIMWI na Haki za Binadamu Bw Emela Paul kutoka mkoani Kagera alitaka kujua kuhusiana sheria ya UKIMWI kuelekeza kupima ni jambo la hiyari na makosa kumpima mtu kwa nguvu na vipi kuhusu watoto wadogo ambao wazazi wao wamekufa kwa UKIMWI na familia inataka kumpima mtoto kujua kama ana VVU au la.

Akitoa ufafanuzi wa kisheria kuhusiana na swali hilo, Afisa Sheria Mwandamizi Miraji alisema mtoto yoyote mwenye umri wa kuanzia mwaka 0 hadi 15 kisheria anakuwa chini ya uangalizi wa mzazi au mlezi na endapo mtoto ataugua mzazi anaweza kumpeleka mtoto hospitali kwaajili ya uchunguzi wa afya yake na hata kumpima VVU kwa kuwa mzazi au mlezi atakuwa anaitekeleza sheria ya mtoto ya mwaka 2009.

Alisema suala la ulinzi na ustawi wa mtoto lipo chini ya mzazi na mlezi nani haki yao kumlinda mtoto kwa namna yoyote ile ikiwemo kumpima afya kwa lengo la kujua maendeleo yake na namna gani ya kumsaidia endapo atakutwa na matatizo ya kiafya.

Alisema sheria inamtaka mtoto mwenye umri wa miaka 15 akitaka kupima UKIMWI lazima apate ridhaa ya maandishi kutoka kwa mzazi au mlezi wake na endapo atakuwa hana kibali hicho hatakiwi kupimwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TACAIDS, Dkt Leonard Maboko ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kukumbuka pia sheria haiwaruhusu kuwaambukiza watu wengine kwa makusudi wakiwemo watoto wadogo na kuwakumbusha kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.

Dkt. Maboko aliwataka pia washiriki wa mafunzo hayo kuwa wawazi wanapoenda kutafuta kazi hasa za ndani kwa kujiweka wazi juu ya afya zao na liwe jukumu la muajiri kuamua kutoa kibarua au la lengo likiwa kuhakikisha unajua namna gani utawalinda watoto wadogo waliopo nyumbani lakini pia kuzuia tabia ya baadhi ya wanaume wanaotumia nguvu kuwataka kimapenzi wadada wa kazi.

Mafunzo hayo ya siku mbili kuhusu Sheria ya UKIMWI na Haki za Binadamu yaliandaliwa na Baraza la Watu wanaishi na UKIMWI Kanda ya Mwanza na kuwashirikisha watu wanaoishi na VVU/ UKIMWI zaidi 60 kutoka mikoa 6 ya Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na 'Mtoto News' mwaka 2019 inaonyesha kuwa watoto wengi walioathirika na UKIMWI wameambukizwa na mama zao wakati wa ujauzito au wakati wa kunyonyesha.
Na Tonny Alphonce, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.