LIVE STREAM ADS

Header Ads

Viumbe hai Ziwa Victoria wako hatarini

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Viumbe hai ikiwemo samaki katika Ziwa Victoria wako hatarini kutokana na taka za plastiki zinazoingia kwa kiasi kikubwa katika Ziwa hilo kubwa duniani linalopatikana katika nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.

Itakumbukwa duniani kote, taka za plastiki ni tatizo kubwa linalosababisha madhara kwa viumbe hai pamoja na uchumi wa mataifa mbalimbali Tanzania ikiwemo kwani taka hizo huchangia kwa kiwango kikubwa uhaba wa mazao ya samaki na hivyo kudhorotesha kipato kwa wananchi na wafanyabiashara kupitia shughuli za uvuvi.
Akizungumza kwenye kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka 2021 lililoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mtafiki kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dkt. Bahati Mayoma alisema duniani kote kumekuwa na kiwango kikubwa cha uzalishaji wa taka za plastiki hadi kufikia tani milioni 350 mwaka 2018 kutoka tani milioni 1.5 mwaka 1970 na uzalishaji unaongezeka kwa kasi zaidi.

“Kati ya kiwango hicho, tani nane hadi 10 huishia chini ya baharini/ ziwani huku tani 150 zikielea majini. Mwaka 2012 aina 800 za viumbe hai wa majini waliathirika na taka za plastiki”alibainisha Dkt. Mayoma.
Miongoni mwa taka za plastiki ambazo Dkt. Mayoma alisema zimeleta madhara makubwa katika maisha ya viumbe hai majini ni pamoja na masalia ya nyavu zinazotekelezwa na wavuvi ziwani/ baharini pamoja na barakoa ambazo baada ya kuibuka janga la Corona uzalishaji wake umekuwa mkubwa huku uteketezaji wake baada ya matumizi ukiwa si wa kuridhisha.

“Katika Ziwa Victoria, jitihada zaidi zinahitajika ili kuokoa uhai wa viumbe hai katika Ziwa hilo. Mwaka 2014 utafiti uliofanyika jijini Mwanza ulibaini kuwa asilimia 95 ya taka za plastiki huishia ndani ya Ziwa Victoria na mwaka 2015 ikagundulika kwamba kila samaki watano, mmoja amemeza bidhaa/ taka ya plastiki.
Katika kongamano hilo, wadau walishauri taka zinazozalishwa kutokana na bidhaa mbalimbali ni vyema zikachakatwa na kutumika tena badala ya kutumika mara moja ambapo hiyo itakuwa njia sahihi ya kupambana na madhara yatokanayo na taka za plastiki. Walisisitiza kuwa taka za plastiki zikitumika kama malighafi na wazalishaji wakaweka utaratibu wa kuzinunua itaongeza hamasa kwa jamii kutozitupa ovyo na badala yake wataziuza ili kujipatia kipato.

“Tunaendelea kutoa elimu kuanzia kwa watoto wadogo mashuleni ili kuwasaidia kubadili tabia na kuhakikisha hawatupi taka ovyo, wanazingatia kanuni za usafi na utunzaji mazingira ambapo hadi sasa tumefikia Shule za Msingi zaidi ya 10” alieleza Afisa Mazingira Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Fanuel Kasenene.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka Juni 05 kwa lengo la wadau mbalimbali kukumbushana umuhimu utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya viumbe hai ambapo kauli mbiu mwaka huu ilikuwa kuhamasisha utunzaji vyanzo vya maji ili kuongoa/ kurejesha mfumo wa Ikolojia.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.