LIVE STREAM ADS

Header Ads

SENGEREMA: Zaidi ya watoto 600 wanufaika na Shirika la Kizazi Kipya

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Katika kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani Agosti 12, 2021, Shirika la Kizazi Kipya limefunga mradi wa kuhudumia jamii inayoishi katika mazingira magumu na UKIMWI katika Wilayani ya Sengerema mkoani Mwanza, ambapo watoto 650 wanaoishi na VVU wamenufaika na mradi huo.

Mradi huo ambao ulikuwa wa miaka mitano uliibua watoto wanaoishi na Virusi vya UKIMWI ambao wengi wao walizaliwa na virusi vinavyosababisha ugonjwa huo ambapo watoto zaidi ya miatano waliokuwa katika hali mbaya ya kiafya wamehudumiwa na kuimarika kiafya.

Muuguzi Iduta Thomasi kutoka Kituo cha Afya Kagunga amesema Shirika la Kizazi Kipya limewasaidia kuwagundua watoto ambao kituo kilishindwa kuwafikia kutokana na umbali uliopo kati ya Kituo na makazi ya wananchi.

Amesema kupitia mradi huo pia waliweza kuwagundua watoto 15 ambao walionekana kuwa na uwingi wa virusi uliosababishwa na kutotumia dawa kwa usahihi na ambapo watoto hao walianzishiwa dawa upya na sasa wanaendelea vizuri.

Amesema utaratibu wa kutembelea nyumba moja baada ya nyingine uligundua kuwa watoto wengi hawakuwa wakipewa dawa kwa usahihi ambapo watoto wote waliokuwa na shida ya unywaji wa dawa wamerudishwa kwenye utaratibu mzuri wad awa.

"Tangu shirika hili lianze kwa kweli tumeona manufaa makubwa kwa sababu hivi sasa watoto wanapatiwa dawa zao kwa wakati na virusi sasa hivi vimepunguza makali na Watoto wapo vizuri" alisema Iduta

Hawa Zawadi ambaye ni Muuguzi kutoka Hospitali ya Busisi amesema changamoto ya unywaji dawa za ARV kwa usahihi bado ni kwa watoto na kwa watu wazima ambapo tatizo la utoro wa dawa limekuwa kubwa.

Zawadi amesema tatizo la utoro wa dawa linafanywa zaidi na kundi la vijana ambao wengi wao wamekuwa wakiacha kutumia dawa baada ya kuona afya zao zikiendelea vizuri bila mashambulizi yoyote ya maradhi.

"Vijana wanatakiwa kujua ni hatari kuacha kutumia dawa kwa usahihi kwasababu kwa kufanya hivyo wanahatarisha afya zao na kutokunywa dawa kwa usahihi husababisha kirusi kuwa sugu na hivyo kuhatarisha afya ya mgonjwa" alisema Zawadi.
Kwa upande wake Afisa Afya na UKIMWI wa Shirika la Kizazi Kipya, Japhari Malima amesema hadi sasa watoto wote ambao wamesajiliwa kwenye mradi huo wanaendelea vizuri.

Amesema tangu waanze mradi huo wa miaka mitano hakuna mtoto ambae ana uwingi wa virusi kwenye damu pia hakuna mtoto amepotea kwenye dawa na hakuna mtoto ambae ametoroka kwenda kuchukua dawa.

Malima amewataka pia wazazi na walezi kuendelea kuwasaidia Watoto wanaoishi na VVU kwa kuhakikisha wanakunywa dawa kwa wakati sahihi na pamoja na kuhakikisha siku ya mtoto kupatiwa dawa katika kituo cha afya anakuwepo.

Siku ya Vijana Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 12 Agosti ili kutoa fursa kwa Serikali na taasisi nyingine kuweka mwangalizo masuala ya vijana ulimwenguni.
Na Tonny Alphonce, Sengerema

No comments:

Powered by Blogger.