LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali yaonya matumizi ya bangi, haitibu C0R0NA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali imewataka wananchi kupuuza taarifa zinazosambazwa kupitia majukwaa mbalimbali hususani mitandao ya kijamii kwamba matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi yanasaidia kupambana na ugonjwa wa C0R0NA.

Tahadhari hiyo ya Serikali imetolewa Januari 18, 2022 na Mkuu wa Mkoa Mwanza, Eng. Robert Gabriel wakati akifungua kikao cha kujadili mikakati ya kupambana na dawa za kulevya kilichowahusisha maafisa wa vyombo vya usalama, Kamati za Usalama ngazi ya Mkoa na Wilaya, Kamati za Afya, viongozi wa dini pamoja na wadau mbalimbali.

“Wanasema bangi inasaidia kutibu Corona, tusipoingilia kati watu wetu kabla ya kuletwa hospitalini watakuwa wanakula bangi, ukiuliza imekuwaje wanakuambia niliona kwenye mtandao” ameeleza Eng. Gabriel akihimiza elimu zaidi kutolewa kwa jamii ili kuondokana na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi.
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Eng. Robert Gabriel.
Eng. Gabriel amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, bado wadau mbalimbali ikiwemo vyombo vya usalama wanapaswa kuhakikisha wanapambana na uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya kwani dawa hizo zina athari kubwa kwa jamii.

Naye Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Gerald Kusaya amewataka wananchi kutoziamini taarifa zinazochapishwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba bangi inatibu Corona akisisitiza kuwa “bangi bado ni haramu, yeyote atakayekamatwa na bangi anatuchuliwa hatua za kisheria”.

Aidha ameongeza kuwa jitihada bado zinahitajika ili kupambana na uzalishaji, uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya ikiwemo bangi akiongeza kuwa takwimu zinaonyesha kuwa kuna zaidi ya watumiaji wa dawa za kulevya laki tano nchini na ambao wanapata tiba katika vituo mbalimbali ni takribani 10,600.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Gerald Kusaya.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.