LIVE STREAM ADS

Header Ads

Halmashauri Mwanza zatakiwa kufufua Mabaraza ya Ardhi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amezitaka Halmashauri mkoani Mwanza kuhuisha mabaraza ya ardhi na nyumba katika ngazi za Vijiji na Kata ambayo yamemaliza muda wake ili yasaidie katika utatuzi wa migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi. 

Mhandisi Gabriel ametoa wito huo Machi 15, 2022 wakati akiwaapisha Wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba kutoka Wilaya za Ukerewe na Mwanza ambao wameteuliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Dkt. Angeline Mabula. 

Aidha Mhandisi Gabriel amezitaka Halmashauri zote mkoani Mwanza kutenga bajeti kwa ajili ya kuwawezesha washauri wa mabaraza ya ardhi na nyumba kupata vitendea kazi na usafiri ili kuwawezesha kutimiza kwa weledi majukumu yao. Pia ameshauri Halmashauri kutoa elimu kwa wajumbe wa mabaraza hayo ili watambue majukumu yao.

Katika hatua nyingine Mhandisi Gabriel amewataka wajumbe wa mabaraza ya ardhi na nyumba kuepuka vishawishi vya rushwa, kutoingia kwenye mitego ya wenye fedha kutaka kuwadhulumu wanyonge na badala yake wasimamie haki huku wakimtanguliza Mwenyezi Mungu kwenye kufanya maamuzi.

Mzee Sijo Maira ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba kutoka Wilaya Ukerewe pamoja na Bi. Blandina Limihagati ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Mwanza wameahidi kutimiza majukumu yao kwa juhudi, maarifa na nidhamu huku wakizingatia sheria na kanuni katika utoaji haki kwa wananchi.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel (kushoto) akishuhudia kiapo cha Mjumbe Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya Ukerewe Sijo Maira (kulia).
Mjumbe Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya Ukerewe Sijo Maira (kulia) akiapa kutumikia nafsi hiyo mbele ya Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel (kushoto). Katikati ni Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya Ukerewe Kato Conrad.
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel (kushoto) akimkabidhi hati ya kiapo Mjumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Mwanza Blandina Limihagati (kulia) baada ya kuapa kutumikia nafasi hiyo.
Mjumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Ukerewe, Muyengi Munubi (kulia) akisaini hati ya kiapo baada ya kuapa kutumikia nafasi hiyo mbele ya Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel (kushoto).
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel (kushoto) akisaini hati za viapo vya Wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba kutoka Wilaya za Mwanza na Ukerewe baada ya Wajumbe hao kuapa.
Wanaoshuhudia ni Mwenyekiti Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya Ukerewe Kato Conrad (katikati) pamoja na Mjumbe Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya Ukerewe Sijo Maira (kulia).

No comments:

Powered by Blogger.