LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC Nyamagana azindua zoezi la utoaji Chanjo ya Polio

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (mwenye nguo ya kitenge) kwa msaada wa wataalamu wa afya akimdondoshea mtoto matone ya chanjo ya Polio ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa kampeni ya kutoa chanjo hiyo wilayani Nyamagana.
***

Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi amezindua rasmi kamapeni ya utoaji chanjo ya ugonjwa wa Polio wilayani humo ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali na wadau mbalimbali wa afya kuwangika watoto dhidi ya ugonjwa huo.

Uzinduzi wa kampeni hiyo yenye kauli mbiu "Kila Tone la Chanjo ya Polio Litaiweka Tanzania Salama dhidi ya Ugonjwa wa Kupooza" umefanyika Ijumatano Mei 18, 2022 katika Zahanati ya Mkolani jijini Mwanza ikitarajiwa kufikia tamati Mei 22, 2022.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Makilagi amesema lengo la kampeni hiyo ni kuongeza Kinga kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili kuwakinga na maambukizi mapya ya ugonjwa wa Polio na kuwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hiyo.

Makilagi amesema baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wagumu kuwapeleka watoto wao kupata chanjo mbalimbali wakidai zinamadhara jambo ambalo si sahihi na kusababisha watoto kupata ulemavu au kupoteza maisha.

"Chanjo hizi hazijaanza kutolewa leo, na kumekuwa na tabia kila chanjo inapotokea inapata ukinzani, niwasihi sana akina mama, msipuuze chanjo hizi kwani ni muhimu katika makuzi ya watoto" amesisitiza Makilagi.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Dkt. Sebastian Pima katika kampeni hiyo wamelenga kuwafikia watoto 92,698 jijini Mwanza na kuhakikisha wanapata chanjo hiyo ya Polio kwani ni muhimu kwao.

Ameowatoa hofu wananchi kuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara hivyo ni vyema wazazi wakajitokeza kwenye Vituo vilivyoainishwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo masokoni, vituo vya mabasi, mashuleni na nyumba za ibada ili watoto wao wapatiwe chanjo hiyo.

"Chanjo hii imekuwa tofauti na chanjo nyingine ambazo zimekuwa zilitolewa kwenye Vituo vya afya pekee, hii ya Polio tunaitoa pia nyumba kwa nyumba hivyo wazazi toeni ushirikiano wa kutosha pindi watoa huduma wanapowafikia kwenye makazi yenu" amesema Dkt. Pima.

Spichiodha Mkongwa ni miongoni mwa waliofika kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo ambapo ameeleza kufurahia baada ya mtoto wake kupatiwa chanjo akisema itamsaidia kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwemo Polio.

"Mimi napenda chanjo kwa sababu ninajua umuhimu wake kwa mtoto hivyo wanawake tunaposikia matangazo ya chanjo tujitokeze kwa wingi ili watoto wetu wapatiwe huduma hiyo na kuwaongezea kinga katika ukuaji wao" amesema Mkongwa.

Naye Mariam Sabi ambaye ni mkazi wa Kata ya Mkolani ameseama chanjo ni haki ya msingi kwa watoto, japo kuna baadhi ya watu wanadhani ni mbaya kutokana na ukosefu wa elimu hivyo Serikali iendelee kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa chanjo.
Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji chanjo ya Polio wilayani humo.
Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Dkt. Sebastian Pima akizungumza kwenye hafla hiyo.
Wananchi wakifuatilia uzinduzi huo.

No comments:

Powered by Blogger.