LIVE STREAM ADS

Header Ads

MPC yatambua jitihada zinazofanywa na FADev

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza (MPC), Edwin Soko amepongeza jitihada zinazofanywa na taasisi ya kuendeleza uchimbaji mdogo wa madini Tanzania (FADev) akisema zitasaidia kuleta mageuzi makubwa katika sekta hiyo.

Amesema jitihada hizo ikiwemo kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo kuhusu masuala ya usalama, utunzaji wa mazingira, kuwaunganisha na taasisi za kifedha pamoja na kuhakikisha wanawake wanashiriki ipasavyo kwenye uchumi wa madini ni miongoni mwa masuala muhimu ambayo yatasaidia kuendeleza sekta ya uchimbaji mdogo wa madini.

Soko ametoa kauli hiyo Agosti 31, 2022 wakati akizungumza kwenye kilele cha warsha ya siku mbili iliyowakutanisha wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuwajengea uwezo ili wasaidie kuleta mabadiliko katika sekta ya uchimbaji mdogo wa madini nchini.

Soko pia amesema baada ya waandishi wa habari kujengewa uwezo na taasisi ya FADev watakuwa na uwezo mkubwa wa kuibua masuala mbalimbali ambayo yanawakabili wachimbaji wadogo wa madini nchini ikiwemo kuhimiza mazingira salama ya kufanyia shughuli zao.

Amesisitiza kuwa ni muda mwafaka sasa waandishi wa habari nchini kujikita katika uandishi wa habari wenye mabadiliko katika jamii hususani katika sekta ya uchimbaji mdogo wa madini ambao tija yake sasa imeanza kuonekana kwa taifa na kwa wachimbaji wenyewe tofauti na mitazamo hasi iliyokuwepi hapo awali

Kwa upande wake Meneja Miradi FADev, Evans Rubara amesema waandishi wa habari ni vyema wakajikita kuangalia maeneo muhimu ya kuandikia habari zinazohusu sekta ya uchimbaji mdogo wa madini ikiwemo changamoto zinazowakabili ili wadau wanaohusika waweze kuzitafutia ufumbuzi hatua itakayosaidia kuwa na uchimbaji mdogo ambao ni endelevu, salama na shirikishi katika jamii.

"Maeneo muhimu ya kuangazia ni afya ya watu kutokana na matumizi ya kemikali ya zebaki ambayo inatumika kwenye kuchenjua dhahabu, afya ya maji ambayo watu wanatumia ili kujua ni kwa kiasi gani shughuli za uchimbaji mdogo wa madini zinaathiri vyanzo vya maji kutokana na sababu mbalimbali kama kemikali ama kukosekana miundombinu muhimu ikiwemo vyoo" amesema Rubara.

Rubara ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa taasisi za Serikali zinazoangazia usalama wa jamii ya wachimbaji wadogo wa madini kutoa ushirikiano wa kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili wasaidie kubaini mapungufu yaliyopo kwenye sekta ya uchimbaji mdogo kwa ajili ya kufanyiwa maboresho.

Akihitimisha warsha hiyo, Katibu Mtendaji wa taasisi ya FADev, Mhandisi Theonestina Mwasha amewahimiza waandishi wa habari kuendelea kufanya kazi kwa weledi, kutafiti kwa kina habari na makala wanazoandaa ili zisaidie kuleta suluhisho la masuala mbalimbali katika jamii.

Katika warsha hiyo, wahariri Kanda ya Ziwa na taasisi ya FADev wamekubaliana kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu ili kusaidia kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya uchimbaji mdogo wa madini nchini.
Mwenyekiti MPC, Edwin Soko.
Katibu Mtendaji FADev, Mhandisi Theonestina Mwasha akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wahariri kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ili wasaidie kutoa Habari za kuendeleza uchimbaji mdogo wa madini nchini Tanzania.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.