LIVE STREAM ADS

Header Ads

DC Nyamagana azidi kutoa elimu ya Sensa kwa wananchi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi amekutana na wananchi katika Kata ya Igoma ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za kutoa elimu ya Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agositi 23, 2022.

Pia Makilagi anatumia fursa hiyo kuwasilisha kwa wananchi taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita kuanzia Julai 2021 hadi Juni 2022, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Igoma Agosti 19, 2022, Makilagi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa wilayani Nyamagana aliwahimiza wananchi kuwa tayari kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi kwani hatua hiyo itasaidia kupata Takwimu Sahihi zitakazotumika kwenye mipango ya maendeleo.

"Msipohesabiwa mtakwamisha mipango ya maendeleo nchini, na katika Wilaya yetu pia kwani bajeti itapangwa bila kuzingatia idadi ya watu, hivyo nawasihi sana toeni ushirikiano wa kutosha katika zoezi la sensa" alisisitiza Makilagi.

Makilagi alisema baada ya zoezi la Sensa kukamilika wananchi wataona faida yake kutokana na mipango ya Taifa itakayowekwa ambayo itakwenda kumjali kila mwananchi.

Aidha aliwaomba wananchi kutowaficha watu wenye ulemavu walio katika kaya zao wakati wa kuhesabiwa ili Serikali itambue idadi yao na kuwajumuisha kwenye mipango ya maendeleo.
Pia Makilagi aliwatoa hofu wananchi kuwa makarani wa Sensa watapita asubuhi ya kuamkia Agosti 23, 2022 kwenye Kaya zao kwa ajili ya kuwahesabu na kwamba watakaohesabiwa usiku kabla ya kupambazuka ni wananchi watakaokuwa wamelala katika maeneo maalumu ikiwemo hotelini, hospitalini, stendi za mabasi, meli na viwanja vya ndege.

Aliwaomba wananchi kuendelea kudumisha amani na kuilinda tunu hiyo muhimu ili zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litamatike kwa Usalama huku nao wakiendelea na shughuli zao za uzalishaji mali.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Igoma, Mussa Ngoro alimshukuru Makilagi kwa kufika katika Kata yake na kutoa elimu kwa wananchi ili kutambua umuhimu wa kuhesabiwa.

Naye James Chacha ambaye ni mmoja wa wakazi wa Kata ya Igoma alisema yuko tayari kuhesabiwa huku akiweka wazi kuwa yeye ana mtoto mwenye ulemavu hivyo zoezi la Sensa litakapofika naye atahesabiwa hatua itakayomsaidia kuwa kwenye mipango ya kupata mahitaji stahiki.
Ratiba ya mikutano ya Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi yenye lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi, kumsikiliza na kutatua changamoto zao pamoja na kuwahimiza kushiriki zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, Agosti 23, 2022.
Na Hellen Mtereko, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.