LIVE STREAM ADS

Header Ads

Mchungaji Moravian: Wakristotoeni sadaka kutimiza uwakili kwa Mungu

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com

 Mchungaji Yona Ezekiel wa Parishi ya Sabasaba ya Kanisa la Moravian Singida mjini, akifundisha somo la Uwakili wakati akiwafundisha waumini (hawapo pichani) wa kanisa hilo katika ibada iliyofanyika leo Januari 29, 2023.

Na Dotto Mwaibale, Singida

WAKRISTO wametakiwa kujitambua na kutoa sadaka na shukurani kwa Mungu ili kutimiza uwakili wa utoaji baada ya kujaliwa kupata fedha,chakula, kazi na vitu vingine.

Wito huo umetolewa na Mchungaji Yona Ezekiel wa Parishi ya Sabasaba Kanisa la Moravian Singida mjini, wakati akifundisha somo la uwakili kwa wakristo katika ibada ya Jumapili iliyofanyika leo Januari 29, 2023.

"Uwakili ni msingi wa kikristo katika kumtolea Mungu matoleo na shukurani mbalimbali baada ya kupata mazao, fedha kutokana na biashara, kazi na mambo mengine yanayofanana na hayo kwani ni lazima kumrudishia Mungu sehemu ya mavuno kwani vitu vyote hivyo vinatoka kwake," alisema Mch.Ezekiel.

Akiwanukuu Mchungaji Dk.Mary Kategile, Mchungaji Profesa Elia Mligo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Njombe, Mchungaji Dk. Tuntufye Mwenisongole, Mchungaji Ekisa Shibanda ambaye anaelezea umuhimu wa mkristo kujitoa na Mchungaji Dk.Ronald Mbao ambaye anasema uwakili ni mkristo anaye pokea mali kutoka kwa Mungu, anailinda,kuitunza, kuitumia na kisha kutoa hesabu ya mali hiyo aliyopewa na kuitunza,  ambapo Mchungaji Dk.Mwenisongole anaeleza kuwa  uwakili ni kumleta mtu karibu kwenye uhusiano na Mungu kupitia utoaji.

Mchungaji Ezekiel alisema kila mkristo anawajibu wa kuwaeleza wengine umuhimu wa suala zima la utoaji wa sadaka na shukurani na kuwa unapotoa sadaka hiyo inapaswa hata mkono wa kushoto kutojua kile ulichokitoa.

Alisema utoaji mzuri ni ule wa kutoa sadaka kwa moyo uliopondeka na mkunjufu na kutoa shukurani kwa siri ili muhusika apate baraka kwa Mungu lakini watu wengi wamekuwa wakimuibia kwa kushindwa kutoa kutokana na kile kikubwa wanachokipata.

Alisema kila mkristo anawajibu wa kuendelea kuwa wakili mwaminifu mbele za Mungu ambaye anatupa mali.

Mchungaji Ezekiel alitaja aina ya sadaka za kumtolea Mungu kuwa ni ile ya kawaida, shukurani na ya pekee.

Aidha,  katika ibada hiyo kanisa hilo usharika wa Sabasaba limeendelea kuwapokea waumini wapya kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Singida ambapo leo hii limempokea Dada Magreth Jacob ambaye ametokea Mkoa wa Katavi.

Mchungaji Ezekiel alitumia ibada hiyo kuwaomba wadau mbalimbali wasaidie michango ya fedha na mali ili kufanikisha ununuzi wa kiwanja kwa ajili ya kujenga Kanisa la Mravian Parishi ya Sabasba kwani hivi sasa wanatumia kibanda kidogo kilicho jengwa kwa miti na kuezekwa kwa bati.

Alisema kwa mtu yeyote atakaye kuwa na wito wa Mungu kusaidia kujenga nyumba hiyo ya ibada bila kujali dini wala dhehebu anaweza kutuma pesa hiyo kupitia Akaunti  Namba 50810046663 Benki ya NMB Kanisa la Moravian Sabasaba Singida mjini au awasiliane na Mchungaji Yona Ezekiel kwa namba 0758-148508.

 Mchungaji Yona Ezekiel wa Parishi ya Sabasaba Kanisa la Moravian Singida mjini, akimpokea Magreth Jacob aliyehamia katika kanisa hilo akitokea Mkoa wa Katavi.
Mchungaji Dk.Ronald Mbao wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa (KMJR)
Mchungaji Dk.Ekisa Shibanda wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini  (KMJK) Rungwe Mbeya.

Mchungaji Dk. Tuntufye Mwenisongole wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi (KMJKM) Mbeya.

Waumini wa kanisa hilo Parishi ya Sabasaba wakiwa kwenye ibada hiyo.
Ibada ikiendelea.
 

No comments:

Powered by Blogger.