LIVE STREAM ADS

Header Ads

Ulinzi na usalama wa watoto bado uko mashakani

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Majivu yatokanayo na moto wa kuni au mkaa pia yanatajwa kutumika kwenye ukeketaji wa Watoto wachanga wa kike bila ya wazazi wa kiume kushirikishwa.

Na Abby Nkungu, Singida
Suala la kuwalinda watoto wa kike walio chini ya miaka minane dhidi ya ukeketaji bado ni changamoto katika Wilaya ya Singida baada ya wazazi na walezi kubuni mbinu mpya ya kutekeleza mila hiyo potofu.

Joshua Ntandu ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la ESTL linalotekeleza mradi wa kupinga ukatili na mila potofu ya ukeketaji dhidi ya watoto wa kike katika wilaya hiyo anasema utafiti wa hivi karibuni unaonesha wazazi na walezi wamebuni mbinu mpya ya kuwasugua sehemu za siri watoto wachanga kwa kutumia ndulele, masizi, majivu au kuwafinya kwa kucha.

“Baada ya kusimamiwa vyema kwa sheria ya kujamiiana inayotaja ukeketaji kuwa kosa la jinai na baadhi ya ngariba kufungwa na mashirika mengi kuingia kwenye mapambano dhidi ya mila hiyo, cha kushangaza baadhi ya wazazi na walezi ambao ndio wenye jukumu la kuangalia ulinzi na usalama wa mtoto wameanza kukeketa kwa siri zaidi ili kukwepa sheria” alisema.

Alieleza kuwa utafiti wa Shirika hilo unaonesha kuwa mjamzito anapokaribia kujifungua huomba ruhusa kwa mumewe kwenda kujitizamia kwa bibi au shangazi ambako ukeketaji huo hufanyika muda mfupi baada ya mtoto kuzaliwa.

Alisema kuwa bado jamii ya Vijijini inakumbatia mila hiyo kwa kuamini kuwa mtoto asiyekeketwa anakuwa na mkosi katika familia yake, ataendekeza umalaya akiwa mkubwa na anaweza kukumbwa na ugonjwa maarufu kwa jina la kienyeji kamaa 'lawalawa' ambao hudhoofisha na kusababisha kifo.

“Kuna hii Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ya miaka mitano kuanzia 2021/22 - 2025/26. Imekuja na masuala mtambuka ya afya, lishe bora, elimu, ulinzi na usalama, nadhani ikisimamiwa vyema kwa kushirikiana nasi wadau wa NGO’s tunaweza kuwa mwarobaini wa hili tatizo kwa kupiga kelele na kuokoa watoto hawa wa miaka 0 hadi 8 wasifanyiwe ukatili huu” alisema na kuongeza kuwa ushirikiano ndio nguzo kuu.

Daktari Bingwa Mshauri wa magonjwa ya Wanawake na Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida, Dk Suleiman Muttani anakiri kuwa ukeketaji kwa watoto wachanga umeshika kasi.

"Kutokana na vichanga hao kuletwa kwenye Vituo vya kutolea huduma ya afya kwa ajili ya kupatiwa huduma mbalimbali, tumebaini jambo hilo ovu na la kikatili wakati wa utendaji wetu wa kazi" alieleza Dk Muttani huku akikanusha kuwepo ugonjwa wa 'lawalawa' kwa watoto, wasichana wala wanawake.

"Kinachofanyika ni kisingizio tu cha jamii ili kutekeleza mila hiyo potofu. Kwa kweli, mila hii ya ukeketaji ni kikwazo cha utekelezaji wa dhana ya ulinzi na usalama wa mtoto mkoani Singida kutokana na athari za kiafya na kisaikosojia kwa watoto kwa muda mrefu na muda mfupi" alisema.

Alitaja athari hizo kuwa ni kutokwa na damu nyingi sehemu za siri au wakati mwingine husababisha kifo na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, Magonjwa ya kuambukiza ya mara kwa mara yanayoweza kumfanya mtoto kuwa tasa anapofikia ukubwani, uharibifu wa mfumo wa njia ya uzazi, matatizo wakati wa kujifungua na kutofurahia tendo la ndoa wakati wa kujamiana.

Hata hivyo, baadhi ya wazazi na walezi wanasema pamoja na kutumia sheria kuwabana wanaoendeleza mila hiyo bado kuna haja ya kuendelea kutoa elimu zaidi juu ya madhara ya ukeketaji kiafya.

“Hii ni mila, ni imani ya watu na imekaa kwenye mioyo yao, haiwezi kutoka kirahisi hasa kwa jamii ya vijijini; hivyo ipo haja ya elimu zaidi” anasema Ruth Daniel mkazi wa Mgori Singida Vijijini na kuungwa mkono na Patrick Mdachi wa Singida mjini ambaye anashauri Serikali iwawezeshe ngariba kupata kipato mbadala kama mikopo ya vikundi ili waache kutegemea ukeketaji.

Tanzania imedhamiria kukomesha kabisa ukatili wa aina zote dhidi ya wanawake na watoto, ikiwemo ukeketaji kama sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya Maendeleo Endelevu 2030.
Masizi ya vyungu nayo ni zana nyingine iliyobuniwa kutumika kuwakeketa vichanga wa kike.
Tunda la Ndulele (pichani) ni moja ya zana mpya iliyobuniwa na wanawake kwa kushirikiana na mangariba katika kutekeleza vitendo vya ukeketaji kwa Vichanga kwa njia ya kificho.
Zana hizi ambazo zimekuwa zikitumika kuwakeketa watoto wadogo wa kike hivi sasa zimeachwa badala yake hutumika mbinu mpya ya kuwasugua sehemu zao za siri kwa kutumia ndulele, majivu na masizi.

No comments:

Powered by Blogger.