LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali inatambua mchango wa mabaharia- DC Masala

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Hassan Masala amesema Serikali inatambua mchango wa mabaharia katika kukuza uchumi wa taifa hivyo itaendelea kuboresha mazingira yao ya kazi.

Masala ameyasema hayo Juni 23, 2023 wakati akifungua warsha ya mabaharia kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Amos Makala iliyolenga kujadili na kuweka mikakati ya kuboresha sekta ya mabaharia.

Amesema kwa kutambua mchango wa mabaharia, Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha na kujenga vivuko na meli na hivyo kutoa fursa ya ajira kwa mabaharia nchini.

Masala pia ametumia fursa hiyo kuwahimiza mabaharia kuwa mabalozi wazuri wa utunzaji mazingira ya maziwa na bahari na kuhakikisha vyombo vya usafiri majini haviwi sehemu ya uchafunzi wa mazingira kama mkataba wa kimataifa wa Marpol unavyoelekeza.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Moses Mabamba amesema shirika hilo limekuwa likitoa elimu ya usalama kwa mabaharia pamoja na kukagua vyombo vya usafiri majini ili kuhakikisha usalama unazingatiwa.

Mabamba amesema mabaharia ni miongoni mwa wadau muhimu kwani asilimia 90 ya mizigo yote duniani inasafirishwa kwa njia ya maji ambapo watoa huduma wakubwa ni mabaharia hivyo sekta hiyo inapaswa kuthaminiwa.

Maadhimisho ya siku ya mabaharia duniani yalianza Juni 22, 2023 ambapo kitaifa yanafanyika jijini Mwanza yakitarajiwa kufikia kilele Juni 25, 2023 yakiambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo maonesho katika uwanja wa Furahisha, kufanya usafi ili kutunza mazingira ya Ziwa Victoria pamoja na mashindano ya riadha.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala akizungumza kwenye warsha ya wadau kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Amos Makalla ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza kuanzia Juni 22-25, 2023.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu TASAC, Moses Mabama akizungumza kuhusiana na wajibu wa shirika hilo kuhakikisha mazingira salama ya vyombo vya majini pamoja na kudhibiti uchafuzi wa mazingira ili kuwa na shughuli endelevu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu TASAC, Moses Mabama akizungumza akizungumza na waandishi wa habari.
Wadau mbalimbali wakiwemo mabaharia wakiwa kwenye warsha ya kujengeana uwezo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani inayofanyika kitaifa jijini Mwanza kuanzia Juni 22-25, 2023.

No comments:

Powered by Blogger.