LIVE STREAM ADS

Header Ads

TASAC yawataka watoa huduma kuzuia uchafuzi wa Ziwa Victoria

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limewataka watoa huduma za usafiri na usafirishaji kuepuka uchafunzi wa bahari na maziwa mbalimbali ikiwemo Ziwa Victoria ili kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira.

Rai hiyo imetolewa Juni 23, 2023 na Kaimu Meneja Mafunzo na Utoaji Vyeti kwa Mabaharia kutoka TASAC, Lameck Sondo wakati wa zoezi la kufanya usafi katika eneo la mto Mirongo jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani.

Sondo amesema baadhi ya taka ikiwemo mafuta ya vyombo vya usafiri majini zina athari kwa viumbe hai hivyo ni vyema watoa huduma wakadhibiti uchafuzi huo kwa manufaa ya viumbe hai na shughuli za kiuchumi.

Amesema TASAC imeungana na wadau wengine kufanya usafi katika dakio la mto Mirongo ambao unamwaga maji yake katika Ziwa Victoria ili kutoa hamasa kwa umma kuona umuhimu wa kutunza mazingira huku pia ikiwa ni utekelezaji kwa vitendo mkataba wa kimataifa wa utunzaji mazingira (Marpol).

"Mkataba huu unatutaka mabaharia kuzingatia utunzaji wa mazingira, kuzuia taka kwenda katika bahari ama maziwa kwani zinaweza kuhatarisha mazalia ya viumbe hai ikiwemo samaki na hivyo kuathiri shughuli mbalimbali ikiwemo za kiuchumi" amesema Sondo.

Sondo ameongeza kuwa asilimia 90 ya mizigo yote inayosafirishwa duniani hutegemea usafiri wa majini hivyo ni vyema jamii ikaungana na wadau wa usafirishaji wakiwemo mabaharia kulinda na kutunza mazingira katika maziwa na bahari.

Mkuu wa Kikosi cha Uzamiaji na Uokozi KMKM Zanzibar, Najma Kalekwa ameshauri mamlaka mkoani Mwanza kuchukua jitihada za kuhakikisha uchafu hauingii katika Ziwa Victoria kupitia mto Mirongo na kushauri tenda kutolewa kwa kampuni itakayokuwa na jukumu la kulinda usafi wa mto huo.

Katibu wa Chama cha Wavuvi Tanzania (TAFU), Jephta Machandalo amesema ni muhimu watoa huduma za usafiri ndani ya Ziwa Victoria, wazalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo zenye vifungashio vya plastiki pamoja na wananchi wakashirikiana pamoja kuhakikisha hawatupi taka ovyo kwani zikiingia katika Ziwa hilo zinaleta athari kubwa ikiwemo kuathiri mazalia ya viumbe hai kama samaki na dagaa na hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi.

 Kwa upande wake Naibu Meya Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Hamidu Said amesema Halmashauri hiyo imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kutenga bajeti kwa ajili ya utunzaji mazingira ya mto Mirongo ili kutoingia taka katika Ziwa Victoria.

Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yameanza Juni 22, 2023 kitaifa jijini Mwanza ambapo kilele ni Juni 25, 2023 yakiambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo za utunzaji mazingira, kutoa elimu kwa jamii na mashindano ya riadha kwa mabaharia.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG 
Kaimu Meneja Mafunzo na Utoaji Vyeti kwa Mabaharia kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Lameck Sondo akizungumza wakati zoezi la kufanya usafi katika dakio la mto Mirongo jijini Mwanza ambao unamwaga maji yake Ziwa Victoria ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani 2023 yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza kuanzia Juni 22-25, 2023.
Kaimu Meneja Mafunzo na Utoaji Vyeti kwa Mabaharia kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ametoa rai kwa wananchi, wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali kuweka miundombinu rafiki ya utupaji taka ili kuzuia uchafuzi wa mto Mirongo hatua itakayosaidia kulinda Ziwa Victoria.
Mkuu wa Kikosi cha Uzamiaji na Uokoaji kutoka KMKM Zanzibar, Najma Kalekwa  akizungumza wakati wa zoezi la kufanya usafi katika mto Mirongo jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazofanyika kuelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Naibu Meya Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Hamidu Said ambaye pia ni diwani wa Kata ya Mirongo ulipo mto Mirongo amesema jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na Halmashauri hiyo kuhakikisha mazingira ya mto Mirongo yanakuwa katika hali ya usafi.
Wadau mbalimbali wakiwemo mabaharia wanaoshiriki Maadhimisho ya Wiki ya Mabaharia Duniani 2023 wakifanya usafi katika eneo la mto Mirongo jijini Mwanza.
Mabaharia wakifanya usafi katika eneo la mto Mirongo jijini Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.