LIVE STREAM ADS

Header Ads

Naibu Waziri wa Afya aridhishwa na maboresho MSD

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai (kulia) akimuelekeza jambo Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel wakati wa ziara ya kikazi akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. John Jingu walipotembelea ofisi za MSD Kanda ya Mtwara.

Na Mwandishi Wetu, Mtwara
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameridhishwa na mabadiliko yanayofanywa na Bohari ya Dawa (MSD) hususani katika utendaji na utekelezaji wa mikataba ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

Dk. Mollel ameyasema hayo akiwa mkoani Mtwara katika ziara ya kikazi akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. John Jingu walipotembelea ofisi za Bohari ya Dawa Kanda ya Mtwara, kujionea hali ya utoaji wa huduma na changamoto ya ufinyu wa ghala unaoikabili kanda hiyo.

Akizungumza na watumishi wa Kanda hiyo, Dk. Mollel amesema, ameridhishwa na mabadiliko yanayofanywa na MSD hususani katika utendaji na utekelezaji wa mikakati ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

Ameongeza kuwa hatua ya Serikali kuazimia kuipatia MSD mtaji ni ya kujivunia, kwani itasaidia kuhakikisha MSD inatekeleza mipango mikakati yake, ikiwemo ujenzi wa maghala na kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana nchini kote.

Sambaba na kutemebelea ofisi za Kanda hiyo, Uongozi huo pia ulizuru eneo la Mikindani mkoani Mtwara, ambalo lipo mkabala na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, mahali linapojengwa ghala jipya la Bohari ya Dawa Kanda ya Mtwara na kujionea jinsi mchakato wa ujenzi wa ghala hilo unavyoendelea.

Dk. Mollel ametumia fursa ya ziara hiyo, kuwapongeza watumishi wa MSD Mtwara kwa juhudi na kujituma kwao katika kuwahudumia wananchi licha ya changamoto ya udogo wa ghala uliopo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jingu amewataka watumishi hao kutobweteka na kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwani serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto zinazowakabili, ikiwemo tatizo la ufinyu wa ghala hali inayosababisha ujenzi wa ghala jipya na la kisasa.

Ameongeza kuwa ziara yao katika Kanda hiyo, ni kudhihirisha kwamba wanatambua changamoto iliyopo, hivyo kwa kushirikiana na viongozi wengine wanaendelea kufanyia kazi changamoto hiyo, ili kupata tatuzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai amesema taasisi hiyo kupitia mpango mkakati wake, iko katika mchakato wa maboresho ya huduma na utendaji kazi, ikiwa ni pamoja na ujezi wa maghala kwenye kanda tofauti nchini.

Amesema hatua hiyo itapanua wigo na uwezo wa MSD katika kuwahudumia wateja wake kikamilifu, kwani itaongeza uwezo wa MSD kuhifadhi bidhaa za kutosha kwaajili ya wateja na kupunguza gharama kubwa za uendeshaji.

Mavere amezitaja Kanda hizo zitakazofikiwa na maboresho ya maghala kuwa ni pamoja na Mtwara, Mwanza, Kagera na Dodoma kwa kuanzia na baadaye kuangalia kanda nyingine zenye uhitaji.
Picha ya pamoja na viongozi wa MSD Kanda ya Mtwara.
Picha ya pamoja na wafanyakazi wa MSD Kanda ya Mtwara.

No comments:

Powered by Blogger.