LIVE STREAM ADS

Header Ads

Wananchi Mwanza watakiwa kuwa na vyombo vya kuhifadhia taka

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wananchi jijini Mwanza wametakiwa kuwa na vyombo maalumu vya kuhifadhia taka katika makazi na maeneo ya biashara ili kurahisisha ukusanyaji wa taka hizo pindi wakala ukusanyaji taka anapopita hatua itakayoimarisha utunzaji wa mazingira ikiwemo vyanzo ya maji.

Rai hiyo imetolewa Jumamosi Septemba 16, 2023 na Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Fanuel Kasenene wakati akizungumza kwenye zoezi la kufanya usafi katika eneo ya mto Mirongo na fukwe ya Ziwa Victoria iliyopo eneo la mradi wa Tampere ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Usafi wa Mazingira Duniani.

Amesema kila mtu anatakiwa kuwajibika katika utunzaji wa mazingira na kuvilinda vyanzo mbalimbali vya maji kwani uchafuzi wa aina yoyote unaweza kusababisha kuua viumbe waishio majini ambao kwa asilimia kubwa ni tegemeo katika kukuza uchumi wa Taifa.

"Sisi kama Halmashauri tumekuwa tukitoa elimu na kufanya kampeni mbalimbali za utunzaji wa mazingira lakini kumekuwa na changamoto kwenye vyanzo vya maji kutokana na taka nyingi zikiwemo za plastiki kuleta athali katika mfumo wa ikolojia ya mto mirongo na ziwa Victoria hali inayosababisha uchafuzi wa mazingira kuongezeka kwa kasi" amesema Kasenene.

Ameeleza kuwa kutokuwa na chombo maalumu cha kuhifadhi taka ni kinyume cha sheria mama ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004 ambayo inatoa wajibu kwa kila mwananchi kuhifadhi taka kwa usahihi.

Kwa upande wake Mtafiti na Mhadhili Msaidizi Shule Kuu ya Sayansi ya Akua na Teknolojia za Uvuvi kutoka Chuo Kikuu Dar es salaam, Bahati Mayoma amesema uchafuzi wa mazingira unaweza kusababisha kuharibu mazalia ya samaki na kupelekea viumbe hai wengine kutoweka.

Amesema kwa Tanzania hali ya taka hususani za plastiki ni changamoto kubwa hivyo linahitaji ushirikiano wa wadau ikiwemo Serikali pamoja na jamii ili kuunga juhudi za pamoja kumaliza tatizo hilo.

"Kutokana na takwimu tulizo nazo makundi makuu mawili ambayo tumeyaona ni sumbufu katika uchafuzi wa mazingira ni chupa za plastiki zinazotumika kama vifungashio vya vinywaji mbalimbali, mifuko pamoja na nyavu za uvuvi" amesema Mayoma.

Naye Afisa Mazingira kutoka shirika la usimamizi wa mazingira na maendeleo EMEDO, Kitoko Laurence amesema zoezi la kufanya usafi linatakiwa liwe endelevu kuanzia kwenye familia, mitaa, kata, wilaya, mikoa na Taifa kwa ujumla.

Maadhimisho ya Siku ya Usafi wa Mazingira Duniani 2023 yamebeba kauli mbiu isemayo "Tuungane Pamoja Kujifunza, Kupanga na Kuhimiza Uimarishaji Huduma za Usafishaji na Udhibiti wa Taka kwenye Ziwa Victoria".
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Afisa Mazingira Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Fanuel Kasenene akizungumza na wanahabari wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usafi wa Mazingira Duniani yaliyofanyika kwa Halmashauri hiyo kushirikiana na wadau kufanya usafi katika fukwe ya Ziwa Victoria pamoja na eneo la mto Mirongo.
Mtafiti na Mhadhili kutoka Chuo Kikuu Dar es salaam, Bahati Mayoma akizungumza na wanahabari wakati wa maadhimisho hayo.
Viongozi wa Halmashaui ya Jiji la Mwanza wakiwa na wadau wa mazingira wakati wakati zoezi la kufanya usafi katika fukwe za Ziwa Victoria ikiwa ni sehemu ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Usafi wa Mazingira Duniani iliyofanyika Septemba 16, 2023.

No comments:

Powered by Blogger.