LIVE STREAM ADS

Header Ads

Ikungi yaunda Kamati za MTAKUWWA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Meneja Miradi wa Taasisi ya Social Action Trust Fund (SATF) Nelson Rutabanzibwa (kulia) akizungumza na wajumbe wa kamati za Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne yaliyoanza Septemba 12, 2023 Wilaya ya Ikungi mkoani Singida na kufikia tamati Septemba 15, 2023.


Na Dotto Mwaibale, Singida
Taasisi ya Social Action Trust Fund (SATF) iliyoanzishwa kwa udhamini wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Serikali ya Marekani (USAID) na kuratibiwa na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kusaidia juhudi za Serikali katika kutoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu waweze kuzifikia ndoto zao limeiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kuunda Kamati za Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika Kata kumi.

Uundwaji wa kamati hizo katika kata hizo umeenda sanjari na wajumbe walioteuliwa kupata mafunzo ya namna ya kuziendesha kamati hizo na kujua utekelezaji wa Mpango Kazi huo wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ambapo wajumbe hao ni ni viongozi kutoka idara mbalimbali za serikali, Asasi za Kiraia, viongozi wa dini na wawakilishi wa makundi ya watu wenye ulemavu, wanafunzi na wanawake chini ya mwenyekiti wake Afisa Mtendaji wa Kata.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Meneja Miradi wa taasisi hiyo, Nelson Rutabanzibwa alisema taasisi hiyo imekuwa ikiwawezesha watoto hao kwa kuwapeleka shuleni, ikiwa hilo halitoshi na kuhakikisha afya zao zinakuwa sawa kwa kuwapatia bima ya afya.

Amesema pamoja na hayo kutokana na watoto hao kutoka katika kaya zenye utete wana hakikisha wanakuwa katika ulinzi na usalama na ndio shabaha kubwa ya kukutana katika kikao hicho cha mafunzo ya kamati hizo za MTAKUWWA zenye lengo la kumlinda mtoto dhidi ya masuala yote ya ukatili.

Amesema kamati hizo zinawasaidia katika miradi yao kuhakikisha watoto wanabaki shuleni kwa sababu vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto vinawafanya washindwe kutimiza ndoto zao kwa kupewa mimba, ndoa za utotoni huku wengine wakiingizwa kwenye ajira wakiwa na umri mdogo na wale wengine ambao -+-+kwa uzembe wao wanaacha tu kwenda shuleni.

Amesema kwa Mkoa wa Singida ipo changamoto kubwa ya watoto kuacha shule kwani walianza na watoto 80 lakini hadi sasa wamebaki na watoto 78 baada ya watoto wawili kutoka kwenye mradi kutokana na sababu mbalimbali kama, mimba, utoro na masuala ya nidhamu.

“Kupitia kamati hizi tunategemea zitaweza kutusaidia kutokana na wajumbe wake kuwa ni polisi ngazi ya kata, maafisa maendeleo, waratibu wa elimu, watendaji wa kata na wengine wote wenye majukumu mbalimbali ngazi ya jamii ambao kwa namna moja yanaweza kusaidia kuwaondolea vikwazo watoto hao washindwe kuendelea na masomo yao” amesema Rutabanzibwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eva Myula akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo aliwataka washiriki kuyatendea kazi hasa kutokana na unyeti wa masuala hayo ya ukatili ambayo yamekuwa ni changamoto kubwa kwenye jamii.

“Niwaombe sana mafunzo mnayopata hapa baada ya kwenda huko kwenye jamii mkayafanyie kazi kwa kuwafichua wanayotenda na kuhakikisha yanafikishwa kwenye vyombo vya dola na kuepuka kupokea rushwa kutoka kwa watuhumiwa kwa lengo la kuwasaidia” amesema Myula.

Myula ametumia nafasi hiyo kulishukuru shirika hilo la SATF kwa kuiwezesha halmashauri hiyo kwa kuunda kamati hizo katika kata hizo kumi ambazo zinakwenda kuongeza mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake.

Mratibu wa Shirika la Oblige for Valnerable Children Tanzania (OVCT) lenye Makao Makuu Puma wilayani Ikungi mkoani hapa, Benard Sungi ambao wanafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi hiyo alisema kwa ushirika wao wameweza kufanya kazi katika Kata nne za Ihanja, Lighwa, Isunna na Kituntu ambapo waliwabaini watoto 80 ambao walikuwa katika mazingira magumu ambao wamepata ufadhili wa masomo kupitia Taasisi hiyo ya SATF.

Amesema kati ya watoto hao wawili waliondoka kwenye mradi na kuwa hao wengine wanaendelea na masomo katika shule mbalimbali za sekondari ambazo amezitaja kuwa ni Isuna, Masinde, Lighwa, Utaho, Miandi na wengine wapo Chuo cha Ufundi Stadi cha FDC kilichopo Manispaa ya Singida.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Mariam Mwandekile alisema mafunzo hayo yamelenga kuzifikia kamati za MTAKUWWA katika kata 10 ambazo ni Puma, Kituntu, Ihanja, Issuna, Dung’unyi, Mtunduru, Sepuka, Makiungu, Mungaa na Lighwa.

Amesema anaamini kabisa kuwa kamati hizo zitakapoanza kutekeleza majukumu na mikakati yao zinakwenda kumaliza kama sio kupunguza kabisa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yao.

Amesema baada ya mafunzo hayo watakwenda kutengeneza mpango kazi na kuanza kuutekeleza ambapo kila baada ya miezi mitatu watakuwa wakitoa taarifa ambayo itaunganishwa na ya wilaya hiyo na kuwa kila mmoja wao atakuwa ni balozi wa kutoa elimu ya kupinga vitendo vyote vya ukatili katika sehemu zao.

Afisa wa Dawati la Jinsia Kituo cha Polisi Wilaya ya Ikungi, Musa Musa amesema katika wilaya hiyo bado kunachangamoto ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vikiwamo vipigo kwa watoto na wanawake, mimba za utotoni, ubakaji, ulawiti na kurithiwa wajane baada ya waume zao kufariki na baadae wakijikuta wakifukuzwa na kunyang’anywa mali walizozichuma na wenza wao.

Amesema kesi nyingi za matukio hayo zimekuwa hazipati ushindi kutokana na mashahidi kushindwa kufika mahakamani kwa sababu mbalimbali zikiwamo za wahusika kupatana na watuhumiwa kwa kupewa fedha hivyo jamuhuri kushindwa kuendelea na kesi hizo kwa kukosa ushahidi.

Amesema desturi ya wajane kurithiwa na ndugu au mdogo wa mume wake baada ya kufariki bado ipo katika wilaya hiyo na inafanyika kwa mtindo wa aina yake kwa familia husika kumchagua mmoja wanafamilia kuwa mwangalizi wa familia ya marehemu ambapo utakuta mjane huyo akiendelea kuzalishwa na endapo atakataa kufanya hivyo atajikuta akifukuzwa huku akinyang’anywa mali alizochuma na mume wake.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii wilayani humo, Flora Temba amesema kuna aina nyingi za ukatili wa kijinsia ambao watu wamekuwa wakifanyiwa hasa watoto na wanawake ambao ameutaja kuwa ni wa kingono, kiuchumi, kisaikolojia, vipigo, kunyang’anywa ardhi.

Temba amesema iwapo atatokea mtu kufanyiwa ukatili huo anaweza kutoa taarifa, kituo cha polisi dawati la jinsia kwa wajumbe wa kamati ya MTAKUWWA, ofisi za Kata, maafisa wa Ustawi na Maendeleo ya Jamii na Huduma ya Mkono kwa Mkono (One Stop Centre) na maeneo mengine ambayo ataona anaweza kupata msaada.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ya MTAKUWWA, Mwinjilisti Isaya Jibu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) akiliwakilisha kundi la viongozi wa dini na mwakilishi wa wanafunzi Salima Juma kutoka Shule ya Msingi ya Damankia walisema kamati hizo zinakwenda kuwa mwiba kwa wale wote wanaoendelea kufanya vitendo hivyo.

Mwinjilisti Jibu ametoa mwito kwa wananchi wa maeneo yote ya kata hizo kutoa taarifa za matukio yote ya ukati kwa wajumbe hao ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua na vyombo husika
Meneja Miradi wa Taasisi ya Social Action Trust Fund (SATF) Nelson Rutabanzibwa, akisisitiza jambo wakati wa mafunzo hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eva Myula akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Mariam Mwandekile, akitoa mada kuhusu MTAKUWWA.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii wilayani humo, Flora Temba, akizungumzia kuhusu aina za ukatili wa kijinsia na namna ya utoaji wa taarifa kwa mtu aliyefanyiwa vitendo hivyo.
Mratibu wa Shirika la Oblige for Valnerable Children Tanzania (OVCT) lenye Makao Makuu Puma wilayani Ikungi mkoani hapa, Benard Sungi, akiwa kwenye mafunzo hayo.
Wajumbe wa MTAKUWWA wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Taswira ya mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja. Aliye chuchumaa ni Mratibu wa Shirika la Oblige for Valnerable Children Tanzania (OVCT) lenye Makao Makuu Puma wilayani Ikungi mkoani hapa, Benard Sungi.

No comments:

Powered by Blogger.