LIVE STREAM ADS

Header Ads

KOTECHA achaguliwa kwa awamu ya tatu kuwa Naibu Meya Jiji la Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Diwani wa Kata ya Nyamagana, Bhiku Kotecha ambaye amechaguliwa kwa awamu nyingine kuwa Naibu Meya wa Jiji la Mwanza.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG

Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza limemchagua diwani wa Kata ya Nyamagana, Bhiku Kotecha kuwa Naibu Meya wa Halmashauri hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja ujayo.

Uchaguzi huo umefanyika Ijumaa Oktoba 27, 2023 ambapo Kotecha amepata kura 20 za ndiyo kati ya wapiga kura 22 huku kukiwa na kura mbili za hapana ambapo ushindi huo, Kotecha anashika nafasi hiyo awamu ya tatu.

“Kura zilizopigwa ni 22, hakuna kura zilizoharibika. Kura za ndiyo ni 20 na kura za hapana ni mbili. Kwa mamlaka niliyopewa naomba kutangaza kuwa Bhiku Kotecha, diwani Kata ya Nyamagana amechaguliwa kuwa Naibu Meya” ametamka msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana, Thomas James.

Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Kotecha amewashukuru madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kumuamini na kumchagua tena kuwa Naibu Meya na kuwaahidi ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Mstahiki Meya Jiji la Mwanza, Sima Costantine amesema ataendelea kushirikiana na Kotecha kuisimamia vyema Halmashauri hiyo na kutekeleza kwa ufanisi shughuli na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Itakumbukwa mwaka 2020/21 Kotecha alichaguliwa kushika nafasi hiyo na kisha ikaenda kwa diwani wa Kata ya Pamba, Rodrick Ngoye mwaka 2021/22 na kisha kuchaguliwa tena mwaka 2022/23.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Sima Costantine (katikati) akizungumza wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo. Kushoto ni Naibu Meya, Bhiku Kotecha na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji Jiji la Mwanza, Aron Kagulumjuli.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Aron Kagulumjuli (kulia) akizungumza wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo. Kushoto ni Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine.
Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana, Thomas James akisoma matokeo ya uchaguzi wa Naibu Meya Jiji la Mwanza.
Diwani wa Kata ya Mirongo, Hamidu Juma akihoji sababu za yeye kutokuwa mgombea wa nafasi ya Naibu Meya wa Jiji la Mwanza baada ya awali kuteuliwa na CCM kugombea nafasi hiyo lakini jina lake halikuwasilishwa Halmashauri na badala yake, likawasilishwa jina la Kotecha.

Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza, Aron Kagulumjuli amesema Halmashauri haiingilii mchakato wa ndani ya chama (CCM).

Hamidu hakuridhika na majibu hayo hatua iliyosababisha kususia uchaguzi huo huku wafuasi wake wakipiga kelele ukumbini hatua iliyowalazimu kutolewa nje na askari mambo wa Halmashauri.
Katika kikao hicho, pia diwani wa Kata ya Igoma, Mussa Ngollo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii huku diwani wa Kata ya Isamilo, Marwa Nyamasiriri akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji.

No comments:

Powered by Blogger.