LIVE STREAM ADS

Header Ads

Ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi inavyowaathiri vijana

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Kulingana na Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya wa 2015-16, zaidi ya asilimia 95 ya vifo vya uzazi vinavyotokea katika nchi zinazoendelea viinasababishwa na ukosefu wa taarifa ya afya ya uzazi na ukosefu wa huduma bora wakati wa kujifungua hususani kwa vijana huku taarifa zikisema vijana wengi nchini wanakutwa na magonjwa ya afya na akili na mwili pale wanapopatwa na magonjwa ya zinaa,mimba za utotoni pamoja na mimba zisizotarajiwa.

Magreth John sio jina lake halisi anasema alishindwa kutumia njia za uzazi wa mpango kwa kuwa rafiki zake wa karibu walimwambia endapo atatumia njia hizo kunauwezekano mkubwa wa kujifungua mtoto mwenye changamoto za kiafya na kiakili.

Mimi nipo chuo mwaka wa pili sasa,nipo kwenye mahusiano tofauti tofauti nasema hivyo kwasababu wanachuo mapenzi yetu hayana mkataba ,leo mpo pamoja kesho mnaachana,niliwahi kusikia kuhusu matumizi ya uzazi wa mpango lakini sikuweza kutumia maana rafiki yangu aliniambia njia hizo zina madhara pindi nitakapo hitaji mtoto naweza kuzaa mtoto mlemavu au mwenye kasoro…niliogopa na nikaamua kutotumia,ila changamoto nazo ni nyingi kunawakati nashika ujauzito ila natumia vidonge ili kuutoa na vitu kama hivyo.

Ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu elimu ya afya ya uzazi inasababisha vijana wengi hususani watoto wakike na mabinti kuingia katika hatari ya maambukizi ya magonjwa ya ngono na UKIMWI.Dkt Agness Steven Marco daktari ambae anahusika na kitengo cha huduma rafiki kwa anasema hakuna mahusiano ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango na mtoto kuzaliwa akiwa na changamoto za kiafya.

Mama mjamzito akiwa na maambukizi ya ngono,maambukizi wa UKIMWI au hakuwahi hospitalini kuanza kliniki hapo mtoto anaweza mtoto akapata maambukizi akiwa tumboni.alisema Dkt Agness

Dkt Agness amesema sababu nyingine ambayo inaweza kusababisha mtoto kuzaliwa akiwa na changamoto ni mtoto kubanwa wakati wa kuzaliwa na kupata majeraha katika kichwa na kwenye ubongo ambapo husababisha ubongo kutokukua vizuri na kupelekea mtoto kuzaliwa akiwa na kichwa maji au kichwa kidogo.

Domitila Faustine msimamizi wa makao kutoka shirika la Wote Sawa la jijini Mwanza anasema Endapo vijana watapatiwa elimu hususani wasichana wanaofanyakazi za nyumbani itawasaidia kujikinga na magonjwa ya zinaa na mimba zisizotarajiwa.

Domitila amesema shirika lao la wote sawa kwa sasa wakishirikiana na serikali ya mkoa wameanza kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana wanaofanyakazi za nyumbani baada ya kubaini kuwa kundi hili lipo kwenye hatari ya kupata mimba zisizo tarajiwa pamoja na magonjwa ya ngono na VVU.

Mfano mwaka jana tulipata kesi zaidi ya 16 za wafanyakazi wa nyumbani ambao walikuwa wakiishi na VVU kati ya hao 6 wameambukiza watu wa pale walipokuwa wakifanyakazi na watano walifariki kwa kukosa matibabu kutokana na kukosa muda wa kwenda hospitali na kupata matibabu.

Kundi lingine ambalo limetajwa kama kundi muhimu la kupatiwa elimu ya afya ya uzazi ni vijana waliopo vyuo vya kati na vyuo vikuu na Kwa kuliona hilo Mhadhiri msaidizi wa chuo cha Mipango Campas ya Mwanza Pelejia Bubelwa ambae pia ni mjumbe wa dawati la njisia amesema wao kama chuo waliona umuhimu na kuanza kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana kwa kuwa tayari wapo na vijana na wengi ambao wamefikia umri balehe na wakati wowote wanaweza kujiingiza katika mahusiano.

Bubelwa amesema tayari jitihada mbalimbali zimeanza kuchukuliwa na vyuo vikuu na vyuo vya kati kwa kushirikiana na shirika la UNESCO wameandaa sera za afya na jinsia ambazo watapatiwa wanachuo ili waweze kupata uelewa wa nini msichana afanye anapopata ujauzito na umuhimu wa kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito.

Tuna online kozi pia ambayo imeanzishwa humo mwanafunzi anaweza kujifunza masuala ya ukuaji,elimu ya afya ya uzazi yeye mwenyewe anajifunza kwa muda mfupi lakini anapata elimu kubwa ambayo inaweza kumuandaa kuwa mama bora au baba bora na kwa hivi sasa hatuwafichi kitu tunawaeleza kila kitu kuhusu mahusiano.alisema Bubelwa

Kutokana na ukosefu huu wa elimu sahihi ya kuhusu afya ya uzazi serikali kupitia vituo vyake vya afya wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi hususani vijana huku mashirika yasiyokuwa yakiserikali nayo yakitoa elimu hii

Miongoni mwa mashirika hayo ni shirika la wanawake Ukerewe kwa kuona umuhimu wa elimu ya afya uzazi kwa vijana wao wameanza kampeni ya kutoa elimu hiyo kwa vyuo vya kati ili kuhakikisha vijana wanajikinga na magonjwa ya zinaa na wanashika ujauzito kwa wakati sahihi kwa manufaa yao na mtoto atakayezaliwa.

Tunaamini tunapowekeza kwa vijana elimu hii ya afya ya uzazi tutakuwa na taifa ambalo lina wazazi wanaojielewa na tutapunguza vitendo vya utoaji mimba holela na pia kupunguza vifo vya wasichana na watoto kwa sababu huyu msichana akitumia njia za uzazi wa mpango atapanga wakati gani ashike ujauzito na wakati gani asishike ujauzito.alisema Sophia Donald mkurugezi wa shirika la wanawake Ukerewe.

Serikali haipo nyuma msikilizaji katika kuhakikisha vijana wanapatiwa elimu ya uzazi wa mpango ili kuwasaidia kuyafikia malengo yao na kuwa na uzazi salama.Mpango Mkakati wa Taifa wa Kuboresha Afya ya Uzazi, Mzazi, Mtoto, na Vijana nchini Tanzania (2016-2020) umeweka mazingira wezeshi ya kupunguza magonjwa, vifo vya akina mama, watoto wachanga, watoto na vijana kwa kutoa huduma bora, endelevu na jumuishi zinazowafikia watu wote katika ngazi mbali mbali za utoaji huduma katika vituo vya afya na kwenye jamii.
Na Tonny Alphonce, Mwanza
Mkurugenzi wa shirika la Sauti ya Wanawake Ukerewe, Sophia Donald.
Msimamizi wa Makao kutoka shirika la WoteSawa, Demitila Faustine.
Mtaalamu wa Afya, Dkt. Agness Steven Marco.
Mdau, Pelejia Bubelwa.

No comments:

Powered by Blogger.