Wafanyakazi Afya Radio Mwanza wapewa mafunzo ya usawa wa kijinsia
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wafanyakazi wa kituo cha matangazo ya redio cha 'Afya Radio 96.9' Mwanza, wamehimizwa kuandaa maudhui ya habari na makala yanayozingatiwa usawa wa kijinsia hatua itakayosaidia pia kuwa na jamii inayoheshimu pia masuala ya usawa katika maamuzi.
Rai hiyo imetolewa Jumanne Agosti 27, 2024 na Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino tawi la Mwanza (SAUT), Nuru Chuo wakati akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa redio hiyo ili kuzingatia usawa wa kijinsia kwenye uandaaji wa maudhui.
Chuo alisema vyombo vingi vya habari nchini vimekuwa havizingatii usawa wa kijinsia kwenye uandaaji wa maudhui ambapo asilimia kubwa sauti za wanawake zimekuwa zikisikika zaidi kuliko sauti za wanawake hatua ambayo imeleta mtazamo hasi kwa jamii kwamba wanawake hawawezi kushiriki kwenye vipindi na mijadala mbalimbali kupitia vyombo vya habari.
"Kama unaandaa taarifa flani, hakikisha unaweka mizania ya watu unaowahoji. Ukihoji wanaume wawili, basi hoji pia na wanawake wawili. Kama una jumla ya taarifa tano kwa siku, leo habari tatu zikihusu wanaume, basi kesho habari tatu pia zihusu wanawake" alishauri Chuo.
Naye Mratibu wa Dawati la Jinsia kutoka Chuo cha Afya Tandabui, Lulu Tawani alisema vyombo vya habari zikizingatia usawa wa kijinsia vitaongeza wafuasi wengi zaidi kwa kuwa makundi yote mawili (wanaume na wanawake) watakuwa wameguswa na maudhui hayo.
"Sauti za aina moja zikisikika zaidi, kuna wasikilizaji wengine utawapoteza. Mfano wanaume wanapenda kufuatilia maudhui yanayorushwa na wanawake na wanawake pia wanapenda kufuatilia maudhui yanayorushwa na wanaume hivyo mkizingatia usawa hadi kwa wafanyakazi, redio yenu itapata wasikilizaji wengi zaidi" alisema Tawani.
Mhariri Mkuu wa Afya Radio Feliciana Manyanda alisema mafunzo hayo yatawaongezea wafanyakazi chachu ya kuzingatia zaidi usawa wa kijinsia kwenye uandaaji wa maudhui, kushughulikia changamoto za kijinsia na kuhakikisha nafasi za maamuzi pia zinakuwa na usawa wa kijinsia.
Kwa upande wake Meneja wa Afya Radio, Idd Juma alisema mafunzo hayo yaliyoshirikisha wafanyakazi zaidi ya 20, yanalenga kuwajengea uelewa wafanyakazi kuhusu masuala la usawa wa kijinsia ili kuwaongezea weledi katika uandaaji wa maudhui bora huku pia wakidhibiti changamoto za ukatili wa kijinsia ndani na nje ya taasisi.
Na George Binagi- GB Pazzo, Mwanza
Meneja wa Afya Radio, Idd Juma akizungumza kwenye mafunzo hayo ya siku mbili kuanzia Agosti 27-28, 2024.
Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino tawi la Mwanza (SAUT), Nuru Chuo akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Afya Radio.
Wafanyakazi wa Afya Radio Mwanza wakifuatilia mada kutoka kwa Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino tawi la Mwanza (SAUT), Nuru Chuo akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo.
Mratibu wa Dawati la Jinsia kutoka Chuo cha Afya Tandabui, Lulu Tawani akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Washiriki wakifuatilia mada kutoka kwa Mratibu wa Dawati la Jinsia kutoka Chuo cha Afya Tandabui, Lulu Tawani.
Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino tawi la Mwanza (SAUT), Frida Mwenda akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Washiriki wakifuatilia mada kwenye mafunzo hayo.
Mmoja wa washiriki akiwasilisha hoja baada ya majadiliano.
Msimamizi wa Vipindi Afya Radio, Esther Baraka akifuatilia kwa umakini mafunzo.
Majadiliano
Tazama BMG TV hapa chini
No comments: