Onesho la SITE 2024 lateka hisia za wengi
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Katika hafla ya kufunga onesho hilo, Jumapili Oktoba 13,2024 kwenye ukumbi wa Mlimani City, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana alieleza kuwa mwitikio wa washiriki umeongezeka, akitaja filamu maarufu ya "The Royal Tour" aliyotengeneza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama kichocheo muhimu.
"Utalii unachangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa, kuanzia pale mtalii anaposhuka uwanja wa ndege, hadi anapohudumiwa na hoteli na kufanya shughuli mbalimbali" alisema Dkt. Chana.
Waziri alisisitiza kwamba ulinzi wa rasilimali za nchi, hususan misitu na mbuga za wanyama, ni muhimu kwa ustawi wa uchumi wa taifa.
"Kila mmoja wetu anawajibika katika kuhifadhi na kutunza mazingira ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya utalii" aliongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania, Balozi Dkt. Ramadhan Dau alionyesha matumaini makubwa kwa mafanikio yaliyopatikana mwaka huu, akisisitiza kuwa ni alama ya mafanikio ya maandalizi ya onesho lijalo, ambalo limefanyika kwa mara ya nane tangu kuanzishwa kwake mwaka 2014.
Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Misitu (TFS), Prof. Dos Santos Silayo alisisitiza umuhimu wa utalii ikolojia, akisema, "Utalii wetu unategemea mazingira safi na yenye kuvutia, ambapo watalii wanapata fursa ya kutembea kwenye misitu, kupanda milima, na kushiriki katika michezo mbalimbali".
Aliongeza kuwa, ikiwa fursa hizi zitatumika vizuri, zitaongeza muda wa kukaa kwa watalii nchini na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa.
Prof. Silayo pia alihimiza Watanzania wote kushiriki katika uhifadhi wa maliasili, akitaja umuhimu wa misitu katika kutoa hewa safi na kulinda mazingira.
"Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa tunatunza mazingira yetu, si tu kwa faida yetu lakini pia kwa vizazi vijavyo" alisisitiza.
No comments: