Rais Samia kuwaongoza wananchi kumuaga Dkt. Ndugulile
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Desemba 2,2024 atawaongoza mamia ya Watanzania katika kuuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile (55).
Dk Ndugulile ambae aliaga dunia usiku wa kumkia Novemba 27,2024 nchini India alikokuwa anapatiwa matibabu, mwili wake unatarajiwa kuletwa machana wa leo Novemba 29,2024 kutoka nchini India.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bunge la Tanzania, mwili wa kiongozi huyo unatarajiwa kufikishwa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) saa 6:35 mchana.
Naibu Spika wa Bunge, Musa Zungu anatarajiwa kuongoza waombolezaji kuupokea mwili huo na utahifadhiwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo.
Ratiba iliyotolewa na Bunge inaonyesha kuwa Desemba 02,2024 saa 12:40 asubuhi mwili wa Dkt. Ndugulile utapelekwa katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Immaculate Upanga kwa ajili ya misa takatifu.
Aidha, saa 2:00 asubuhi mwili utaondolewa kanisani hapo kwenda Viwanja vya Karimjee kwa ajili ya salamu za mwisho za kitaifa zitakazoongozwa na Rais Samia.
Mwili wa Dkt. Ndugulile utapumzishwa Desemba 3, jijini Dar es Salaam.
#KAZIINAONGEA
No comments: