Wachimbaji wadogo Nyang'hwale mkoani Geita wamwangukia Rais Samia
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Ifugandi, Kata ya Busolwa, Wilaya ya Nyang'hwale mkoani Geita.
Na Hellen Mtereko, Geita
Wachimbaji wadogo wa dhahabu katika machimbo ya Ifugandi, Kata ya Busolwa, Wilaya ya Nyang'hwale mkoani Geita, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kupata utatuzi wa mgogoro baina yao na mwekezaji wa kampuni ya Sailats Investment baada ya machimbo hayo kufungwa kutokana na mgogoro huo.
Wachimbaji hao walitoa ombi hilo Alhamisi Novemba 07, 2024 kufuatia zuio walilowekewa tangu Oktoba 31, 2024 la kutoendelea na shughuli za uchimbaji katika machimbo hayo.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji hao, Mwenyekiti wa chama cha ushirika wa wachimbaji wadogo wa dhahabu Ifugandi, Zabron Mesanga alisema kitendo cha kuzuiliwa kuendelea na shughuli ya uchimbaji kimeathiri uchumi wao na wa wananchi wanaozunguka eneo la machimbo.
"Chama hiki kinawanachama 175 na tuna watu zaidi ya 2,000 ambao wanafanya shughuli ya uchenjuaji madini na wananchi zaidi ya 10,000 wanategemea mgodi huu kwa ajili ya kujipatia kipato hivyo Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia ione namna ya kutusaidia kwani kwa sasa hali ya uchumi ni ngumu sana" alisema Mesanga.
Alisema walianza kuchimba mwaka 2012 ilipofika mwaka 2019 wakashauriwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyang'wale kuanzisha chama cha ushirika ili waweze kupata leseni.
"Tulisajili kikundi chetu Agosti 30, 2024 baada ya hapo tukaanza kufuatilia leseni, tumeanza kupambania leseni tukakumbana na mwekezaji kampuni ya Sailats akiwa anafuatilia pia leseni ya uchimbaji katika eneo hili na akaonekana ana haki ya kupewa leseni kwa kigezo cha kuwa alikuwa na leseni za utafiti wa eneo hilo tangu mwaka 1994. Tunaomba tupate suluhu ili tuweze kujua tutanufaikaje na mgodi huu" alisema Mesanga.
Naye Ruth Yombo ambaye ni miongoni mwa wachimbaji wadogo, alisema anapitia wakati mgumu wakuhudumia familia yake kwani kwa sasa anafanya kazi za mgahawa ambapo kwa siku analipwa 2,000 fedha ambayo haikidhi mahitaji yake.
"Mimi ni mjane nashindwa kuhudumia familia yangu kwa sasa, kipato changu kimeshuka hivyo tunamuomba Rais Dkt.Samia atusikilize kilio chetu ili tuweze kuendelea na kazi ya uchimbaji" alisema Yombo.
Kwa upande wake Msafiri Mathias ambaye pia ni mchimbaji mdogo alieleza kuwa endapo suala lao halitapatiwa ufumbuzi hawatakuwa tayari kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.
Mwakilishi wa kampuni ya Sailats Investment ambaye pia ni Meneja mgodi wa Ifugandi Edward John alisema wachimbaji hao wamezuiliwa kuchimba kutokana na duara kutokuwa na usalama.
"Duara zimefungwa timba kwa asilima asilimia 20 na asilimia 80 haijafungwa hivyo watu wanaohusika na madini wakahofia usalama wa wachimbaji hao ndio maana wakachukua uamuzi wa kuwakataza kuendelea na shughuli za uchimbaji" alisema John.
Mwenyekiti wa chama cha ushirika wa wachimbaji wadogo Ifugandi Wilaya ya Nyang'hwale mkoani Geita, Zabron Mesanga akizungumzia kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji katika machimbo ya Ifugandi.
Mashine iliyokuwa ikiwasaidia kuchimba kabla ya kusimamisha shughuli za uzalishaji katika mgodi wa Ifugandi.
Mwonekano wa mebele wa ofisi ya chama cha ushirika cha wachimbaji wadogo Ifugandi wilayani Nyang'hwale.
No comments: