LIVE STREAM ADS

Header Ads

Watendaji Jiji la Mwanza wakumbushwa wajibu wao

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkurugenzi Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo tawi la Shinyanga, Dkt. John Kasubi akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Watendaji wa Mitaa na Kata Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
***

Halmashauri ya Jiji la Mwanza imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa ili kuwawezesha kufanya kazi kwa weledi na mipaka bila kuingiliana.

Afisa Utumishi wa Halmashauri hiyo, Leonard Majuto amesema pia mafunzo hayo yatawasaidia watendaji wa Kata na Mitaa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma huku wakishirikiana na viongozi wengine wakiwemo Madiwani kusimamia miradi ya maendeleo.

“Tayari tumetoa mafunzo kwa Wenyeti na Wajumbe wa Serikali za Mitaa hivyo tunaamini sasa kwa pamoja wataenda kusimamia shughuli za Serikali, kuibua miradi ya maendeleo na kutatua migogoro ya wananchi” amesema Majuto.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiwemo waliopata ajira mpya ambao ni Olaf Ndunguru na Christina Buha wamesema yatawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi na kuwezesha maendeleo kwa wananchi huku watendaji waliokuwa kazini akiwemo Caroline Masanja akisema yamewaonezea ari na nguvu mpya kazini.

Mafunzo hayo yametolewa na wakufunzi kutoka chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kampasi ya Shinyanga ambapo Mkurugenzi wa chuo hicho, Dkt. John Kasubi akisema yatawasaidia watendaji kushirikiana na wananchi badala ya kujiona mamwinyi kazini.

“Pia tumewafundisha matumizi ya TEHAMA na umakini wa kutovujisha siri za ofisi. Lakini pia kuwakumbusha kufanya maandalizi sahihi ya kustaafu ili kuwa na maisha mazuri baada ya utumishi wa umma” amesema Meneja Rasilimaliwatu chuo cha Hombolo tawi la Shinyanga, Boniphace Michael.
Tazama BMG TV hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.