LIVE STREAM ADS

Header Ads

Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wurzburg kuimarisha utunzaji wa mazingira

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kushirikiana na Jiji la Wurzburg kutoka Ujerumani imekabidhi vifaa vya usafi katika Shule ya Sekondari Fumagila vitakavyowasaidia kuimarisha usafi na kutunza wa mazingira katika shule hiyo.

Akikabidhi vifaa hivyo, Mratibu wa Mahusiano baina ya Jiji la Mwanza na Jiji la Wurzburg, Billy Brown ametaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na majembe, mapaka, matoroli, mabuti na vikusanyia taka.

Alisema wameweka mpango madhubuti na endelevu kwa ajili ya kuendeleza kuhusisha shule za Jiji la Mwanza na jamii ili kuhakikisha wanatunza mazingira kwa kupanda miti ili kukabiliana na changamoto ambazo zinatokana na mabadiliko ya tabianchi.

"Tutashirikiana kwenye ajenda hii ya kuhifadhi mazingira, usafi wa mazingira pamoja na kuhifadhi Bayonowayi na kuhakikisha jamii inakabiliana na mabadiliko ya tabianchi" alisema Brown.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Fumagila, Mwal. Dotto Daniel alipongeza ushirikiano baina ya Jiji la Mwanza na Jiji la Wurzburg ambapo aliahidi kusimamia vyema vifaa hivyo ili kuleta tija iliyokusudiwa.

"Tutaboresha mazingira yetu kutokana na vifaa hivi, awali tulikuwa na changamoto hivyo naamini vitatusaidia kuimarisha usafi wa mazingira hapa shuleni" alisema Mwl. Daniel.

Nao baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Hafsa Rashid na Leah Burugu walitoa shukurani zao baada ya kupokea vifaa hivyo wakisema vitawasaidia kufanya usafi kwa wakati na kuondokana na adha iliyokuwepo.
Na Sadam Zinga, Mwanza
Mratibu wa Mahusiano baina ya Jiji la Mwanza na Jiji la Wurzburg, Billy Brown  akimkabidhi vifaa vya usafi Mkuu wa Shule ya Sekondari Fumagila, Mwl. Dotto Daniel (kushoto).
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Fumagila jijini Mwanza wakiwa na vifaa mbalimbali vya usafi vilivyotolewa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa ushirikiano na Halmashauri ya Jiji la Wurzburg.

No comments:

Powered by Blogger.