LIVE STREAM ADS

Header Ads

Tume Yaahidi Mazingira Rafiki kwa Walemavu Katika Uchaguzi Mkuu

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Na Cathbert Kajuna, Kajunason Blog.

DAR ES SALAAM – Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, ametoa wito kwa watu wenye ulemavu nchini kuwa mabalozi wa amani na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, kwa kuhakikisha wanawahamasisha wenzao kujitokeza kupiga kura na kulinda utulivu wa taifa.

Jaji Mwambegele alitoa wito huo leo, Julai 31, 2025, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Tume na watu wenye ulemavu kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Jaji Mwambegele alisema kuwa katika kipindi cha kampeni huwa kunashuhudiwa joto la kisiasa kutokana na baadhi ya wananchi kukosa uvumilivu wa kisiasa, hali inayoweza kuhatarisha amani ya nchi.
“Kupitia majukwaa yenu, mna nafasi ya kuwa sehemu ya walinzi wa amani. Tunawasihi kuwaelimisha wenzenu wenye ulemavu kuwa makini na kuhakikisha kuwa hawawi chanzo cha kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu katika kipindi cha kampeni,” alisema Jaji Mwambegele.

Alieleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatambua mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika mchakato wa kidemokrasia, na ndiyo sababu imeandaa kikao hicho mahsusi ili kutoa taarifa, kupokea maoni na kuhakikisha ushirikishwaji wao unazingatiwa katika kila hatua ya maandalizi ya uchaguzi.

Aidha, Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa ratiba rasmi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 tayari imetangazwa, ambapo utoaji wa fomu za kugombea urais utaanza Agosti 9 hadi 27, 2025. Uteuzi wa wagombea wote utafanyika tarehe 27 Agosti, huku kampeni zikianza Agosti 28 na kuhitimishwa Oktoba 28 kwa Tanzania Bara na Oktoba 27 kwa upande wa Zanzibar.
Kuhusu mazingira rafiki ya kushiriki uchaguzi, Jaji Mwambegele alisema kuwa Tume imekuwa ikichukua hatua kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata taarifa kwa wakati na kushiriki bila vikwazo, ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu rafiki katika vituo vya kupigia kura.

Akiendelea, alieleza kuwa hadi sasa taasisi 164 zimesajiliwa kutoa elimu ya mpiga kura, huku taasisi 88 (76 za ndani na 12 za kimataifa) zikiwa zimesajiliwa kwa ajili ya uangalizi wa uchaguzi.
“Tume itafanya kazi kwa karibu nanyi ili kuhakikisha elimu ya mpiga kura inawafikia walemavu wote na kwamba wanajua haki yao, wajibu wao, na namna ya kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la uchaguzi,” alisema Jaji Mwambegele.

Vilevile, aliwataka watu wenye ulemavu waliopata vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na miongozo ya Tume katika kutekeleza majukumu yao, huku akisisitiza kuwa Tume itaendelea kusimamia uchaguzi kwa kuzingatia Katiba, sheria, na taratibu ili kuhakikisha uchaguzi wa mwaka 2025 unakuwa huru, wa haki, na wa kuaminika.

“Kauli mbiu yetu inasema ‘Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura’. Tume inatambua na kuthamini nafasi yenu na itaendelea kuwashirikisha katika hatua zote za mchakato huu,” alihitimisha.

No comments:

Powered by Blogger.